Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti wa Chadema Ruangwa akamatwa kwa kupandisha bendera

80671 Chademapic

Fri, 18 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Erasmus Libaba amekamatwa na kuhojiwa kwa kosa la kupandisha bendera ya chama hicho katika barabara ambayo viongozi wa Serikali wanapita katika msafara.

Tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita ambapo Libaba alikamatwa na polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa kisha kuwekwa ndani hadi alipoachiwa siku iliyofuatia yaani Jumatano.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu mkasa huo, Libaba alisema wamekuwa na utaratibu wa kupandisha bendera za Chadema asubuhi na kuzishusha jioni, “kwani tukiziacha, watu wasiojulikana wanazishusha usiku.”

“Hawashushi tu bali wanavunja na mashina yetu yanayotumika kushusha bendera,” alisema Libaba.

Mwenyekiti huyo alisema, “siku moja kabla ya viongozi wa serikali kuja Ruangwa, vijana wetu walizuiwa kupandisha bendera lakini mimi nikawaambia kwa nini watuzuie wakati Katiba na sheria za nchi zinaturuhusu.”

“Sasa...Jumanne ilikuwa kama saa 4 asubuhi, tukiwa kijiweni kwetu Mitope, alikuja mkuu wa wilaya akiwa na polisi na watu wengine, vijana walipoona vile walikimbia nikabaki mimi.”

Pia Soma

Advertisement
“Wakaja kuniuliza nani amepandisha bendera, mimi nikasema vijana wangu na mimi ndiyo mwenyekiti, wakazichukua bendera na kunipa kisha wakanipandisha kwenye gari na kunipeleka kituo cha Ruangwa,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema, “nilikaa kituoni hadi jana (juzi) saa saba hivi waliponihoji kwa nini nilipandisha bendera za Chadema katika barabara ambayo viongozi wa Serikali wanapita, mimi nikawaambia sioni kosa lolote.”

“Sasa nikajiuliza kwani kuna kosa kupandisha bendera. Waliniachia na kunitaka kuripoti tena kituoni Jumatatu. Lakini nimweleze mkuu wa wilaya afuate katiba na sheria za nchi, Chadema ni chama kimesajiliwa, kinaruhusiwa kupandisha bendera zake,” alisema.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini aliamuru akamatwe, Mkuu wa Wilaya, Mgandilwa alisema “suala hilo ni la kimahakama.”

Mwananchi lilipotaka kujua zaidi hadi anatoa amri kulikuwa na viashiria gani, mkuu huyo wa wilaya alisema suala hilo linaendelea kushughulikiwa.

Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema kitendo hicho kinapaswa kukemewa.

Dk Mashinji alisema wanasubiri Libaba afikishwe mahakamani na “kama watamshitaki kwa kupandish bendera za Chadema itakuwa kesi ya kuvutia na nitapenda mawakili wangu wawepo.”

Chanzo: mwananchi.co.tz