Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenge wa Uhuru wamuweka matatani DED Arusha

18023 Pic+mwenge TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha limetakiwa kuandika barua kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Charles Kabeho kueleza zilipo Sh468,000 zilizopelea katika mradi wa ujenzi wa madarasa manne katika shule ya sekondari Arusha.

Mradi huo wa madarasa manne uliozinduliwa na Mwenge wa uhuru ulizua hali ya sintofahamu mara baada ya mkuu wa shule ya sekondari Arusha, Christopha Malamsha kusoma taarifa za mradi huo kugharimu jumla ya Sh78.39 milioni.

“Mradi huu ulioanza Desemba mwaka jana na kukamilika mwaka huu uligharimu jumla ya Sh78.39 milioni ukiwa na lengo la kuondoa changamoto ya ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa shuleni hapo baada ya Sera ya Elimu bure,” amesema Malamsha

Baada ya  kukabidhi taarifa hiyo leo Septemba 18,2018 ziara ya kiongozi huyo wa mwenge kitaifa Kabeho ulianza kwa ukaguzi wa madarasa ukiongozwa na mkuu wa wilaya ya Arusha Fabian Daqarro na mkurugenzi wa jiji Dk Maulid Madeni.

Kabeho baada ya kutembelea madarasa hayo alisema hali ya mradi huo unatia shaka na thamani ya fedha iliyotolewa na kulazimika kuomba ramani ya mradi huo uliobainisha mradi kugharimu Sh77.93 milioni hali iliyotofautiana na taarifa ya awali  iliyosema mradi umegharimu Sh 78.93 milioni.

Mhandisi wa jiji Erasto Eshuzza akijibu hoja ya kuchanganya taarifa alisema hajui lolote katika taarifa iliyosomwa na mkuu wa shule hiyo kwa niaba ya mkurugenzi wa jiji kwani ramani aliyonayo ni ya wizara ya elimu ambayo pia aliikabidhi.

“Sijui hata hii taarifa na ramani wameipata wapi hawa, labda itakuwa wamefanya editing (wamehariri) tu, maana taarifa niliyonayo iko kwenye ukurasa wa kitabu cha wizara ya elimu hivyo naomba radhi kwa hilo uturudishie hii iliyokosewa na uchukue hii ambayo ni sahihi,” amesema Erasto.

Hata hivyo, baadaye baada ya kiongozi wa mwenge  kufanya ziara fupi katika maduka kadhaa ya vifaa vya ujenzi alipata bei halisi ya vifaa vilivyotumika katika mradi huo na kuridhishwa na taarifa ya pili kuwa mradi uligharimu Sh77.93 milioni.

“Nimekubali sasa kuzindua mradi huu wa madarasa manne kwa taarifa ya pili niliyopewa kuwa umegharimu milioni 77.93 ila kwa sababu nilipokea taarifa ya kwanza kuwa uligharimu milioni 78.39 na fedha zimetolewa kutoka kwenye vyanzo vyetu vya ndani vya halmashauri ya jiji," alisema Kabeho

"Nataka mkurugenzi aniandikie barua zilipo hizo fedha au matumizi ya hizo fedha zilizobaki Sh468,000 ndiyo tutaelewana maana niliapa kufanya kazi hii mbele ya Mungu na Rais wangu kwa ukweli hivyo sitaki kudanganya wala kudanganywa.”

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha alikubali kuandaa barua hiyo ya taarifa ya maelezo zilipo fedha hizo.

Chanzo: mwananchi.co.tz