Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, imesema imejipanga kuboresha sekta ya usafirishaji nchini kwa kupanua mradi wa ujenzi wa barabara za mwendokasi ili kupunguza adha za usafiri jijini Dar es Salaam.
Haya yamewekwa wazi na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Godfrey Kasekenya, leo Novemba 05,202 katika Kongamano la Miundombinu linalofanyika jijini Dar es Salaam.
Kasekenya amesema kuwa hadi sasa Wizara hiyo ina jumla ya awamu sita za ujenzi wa barabara hizo huku lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika barabara za mjini.
"Tuna awamu sita za ujenzi wa barabara za mwendokasi. Awamu ya kwanza tumeshaikamilisha ambayo ni magari yanayotoka Morocco mpaka katikati ya jiji.
Aidha amesema kuwa Serikali imedhamiria kupunguza foleni na pia kujipatia kipato kwa kuanzisha mradi huu na kuwa hivi sasa wapo kenye ujenzi wa awamu ya pili.
"Awamu ya pili ndiyo tunajenga barabara za kutoka Mbagala mpaka Chang'ombe, Kawawa mpaka Magomeni na tutakuja kujenga pia mwendokasi kutoka katikati ya jiji kwenda Gongo la Mboto" Amesema Kasekenya.
Ameongeza kusema kuwa miradi yote hii imetekelezwa katika kipindi hiki cha Uhuru,
"Haya yote yamefanyika wakati huu wa Uhuru" Amehitimisha Naibu huyo.