Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanza wampa ‘tano’ Samia kwa hatua bandarini

4dbc62aac4fe7bd94a98f0ad4dc8ca27.png Mwanza wampa ‘tano’ Samia kwa hatua bandarini

Wed, 31 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKAZI wa Mwanza wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanza vyema kuiongoza nchi baada ya kupokea ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na kufanya maamuzi ya kumsimamisha mkurugenzi mkuu wa Bandari.

Akizungumza na HabariLEO, mkazi wa kata ya Nyegezi, Edwin Soko alisema Rais Samia alifanya vyema katika maamuzi yake.

''Rais Samia alifuata misingi ya utawala kwa kufuata sheria na taratibu'' alisema Soko.

Alisema Rais huyo ameelezea vizuri pasipo kuficha na kuweka wazi kuwa kuna shida kwenye ripoti hasa ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

''Ripoti ya CAG imempa nafasi mama kuona kuwa mambo hayapo sawa ndio maana kaagiza kumsimamisha kazi mkurugenzi wa bandari,'' alisema Soko.

Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Erick Ambakisye alisema maamuzi ya Rais yamewapa Watanzania nguvu na maamuzi yake ya kupata taarifa kupata taarifa ya matumizi ya serikali ya kuanzia Januari mpaka Machi.

''Mama Samia ni tumaini jipya kwelikweli. Kikubwa tumuombee ashikilie msimamo wake wa kizalendo,'' alisema Ambakisye.

Mkazi wa kata ya Mkuyuni, David Paul alisema Rais amejibu kwa kiasi kikubwa swali lililokuwa vichwani kwa Watanzania na wa Mataifa mengi kuwa je atakabiliana na vitendo vya kifisadi kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Rais John Magufuli.

Alisema kwa muda mfupi wa dakika 20 za hotuba yake ameonesha kweli ni Rais Shupavu na ataangamiza ufisadi.

Alisema wengi wamefurahi kitendo cha kuwaamsha Takukuru kwa baadhi ya mambo yao kutokufanya vyema hasa kuingilia majukumu yasiyo yao kama kudai madeni, kubambikiza kesi huku akisisitiza kesi zenye ushahidi wa uhakika kufikishwa mahakamani ili kuleta heshima kwa serikali kwa kushinda kesi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz