Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanry azungumzia vibwagizo na vijembe katika hotuba zake

34623 Mwanri+pic Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amefunga mwaka 2018 akiwa kiongozi aliyevutia zaidi katika mitandao ya kijamii kutokana na kauli anazotoa wakati akizungumza na watendaji, lakini nyuma ya kauli hizo kuna anacholenga kutekeleza.

Miongoni mwa kauli zake zilizoibua mijadala katika mitandao hiyo ni pamoja na ile ya “injinia soma hiyooo”, “sukuma ndani”, “fyekelea mbali” na ile ya wakulima “tatizo betri.” Nyingine ni “nyoosha mkono, jifanye tu kama unajikuna.”

Mwanri aliyewahi kuwa naibu waziri wa Tamisemi katika Serikali ya Awamu ya Nne, alikuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa 13 walioteuliwa na Rais John Magufuli kuongoza mkoa huo Machi 13, 2016.

Katika mahojiano na Mwananchi, Mwanri anasema sababu ya kutumia lugha za ukali na mifano wakati wote huchagizwa na matabaka ya viwango tofauti vya wananchi kupokea na kuyafanyia kazi maelekezo yake. “Unajua mimi staili yangu ya kufanya kazi huwa ninaamini kwenye jambo, nitatumia nguvu ile ambayo Mungu amenipa nikiamini kwamba wananchi wa kawaida wana viwango tofauti vya uelewa, hivyo nachukulia kama niko darasani na wanafunzi wanaotaka kueleweshwa jambo,” anasema Mwanri anapofafanua kwa nini amekuwa akitumia lugha ya mifano, vijembe na vitisho katika hotuba na maelekezo anayotoa kwa wananchi au watendaji wa kada mbalimbali.

“Wako wanaoelewa haraka, wako wanaoelewa kwa kiasi, wako ambao inachukua muda kuelewa na wapo ambao hawaelewi kabisa hata lugha yenyewe ninayotumia, kwa hiyo ili waweze kuelewa inabidi nitumie njia kama hizo za mifano lakini kwa sasa wananchi wa mkoa wangu wa Tabora tunaelewana sana.”

Akimzungumzia Mwanri na mtindo wake wa uongozi, Profesa Mohammed Bakari wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema faida ya uongozi wa aina hiyo ni uhamasishaji mzuri katika maendeleo ya wananchi.

“Hii tunaita populism leadership style (umaarufu wa kiuongozi), kwa bahati mbaya anaweza kubebwa na media (vyombo vya habari) bila kuwa na matokeo mazuri kwa wananchi anaowaongoza, lakini wako viongozi watulivu na hufanikiwa zaidi katika mipango ya maendeleo bila umaarufu wa vyombo vya habari,” alisema.

Umaarufu wa Mwanri umeibuka zaidi baada ya baadhi ya kauli zake kugeuzwa vibwagizo katika vipindi vya burudani redioni na mitandaoni.



Chanzo: mwananchi.co.tz