Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ametoa siku 49 Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora (Tabotex) kuboresha ufanisi wake katika uzalishaji vinginevyo atashauri kirudishwe serikalini.
Akizungumza leo Jumapili Novemba 18, 2018 katika maadhimisho ya miaka mitano ya halmashauri ya wilaya ya Kaliua, Mwanri amesema hawezi kukaa kimya wakati kiwanda kinasuasua.
Amebainisha endapo kiwanda hicho kitaendelea kusuasua ikifika Januari mosi mwakani ataiandikia barua Serikali kushauri kirudishwe kwa umma.
"Kiwanda hiki kina uwezo wa kuajiri kwa shifti watu 1,050 kwa siku. Ni chanzo kizuri cha ajira. Lazima wananchi wanufaike na kiwanda hicho kwa kupata ajira," amesema.
Mwanri amesema mkoa wa Tabora umeandaa kongamano la fursa za uwekezaji kuanzia Novemba 21 hadi 23 na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa ndiye anayetarajiwa kulizindua.
Maadhimisho hayo yatafanyika katika ofisi ya halmashauri hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, watumishi na wananchi.