Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwandishi wa habari wa MCL afariki dunia

14411 Pic+mwananchi TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya/Dar. Mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Raymond Kaminyoge amefariki dunia.

MCL ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti, The Citizen na inamiliki mtandao wa MCL Digital.

Matilda Kaminyoge, dada wa Raymond alisema jana kuwa kaka yake alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Alisema awali Raymond alikuwa akipata matibabu katika hospitali mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa miezi mitatu kabla ya kuhamishiwa Mbeya kwa ajili ya uangalizi wa karibu zaidi wa ndugu zake.

“Familia tulipata taarifa kuwa ni mgonjwa, tulifanya utaratibu wa kumfuata Dar es Salaam, Agosti 11 kwa ajili ya usimamizi wa karibu wa matibabu. Agosti 17 tulimpeleka hospitali ya rufaa ambako alilazwa mpaka mauti ilipomfika,” alisema Matilda ambaye ni msemaji wa familia.

Alisema Raymond alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na kisukari. Alisema mazishi yatafanyika leo katika makaburi ya Iwambi jijini Mbeya.

Matilda alisema Raymond ameacha mjane na watoto watatu.

Aliushukuru uongozi wa MCL kwa kujitoa kwa hali na mali kuchangia fedha kwa ajili ya matibabu na kuwa na mawasiliano ya karibu na familia.

Meneja Mauzo na Uendeshaji wa MCL, Arnold Kimanganu akizungumza na familia kwa niaba ya kampuni alisema Mwananchi imepoteza mtu muhimu katika tasnia ya habari.

“Uongozi wa kampuni na wanahabari wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Kaminyoge, alikuwa mtu muhimu, mcheshi na aliyejituma katika utendaji wa kazi,” alisema Kimanganu.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Bakari Machumu katika rambirambi kwa msiba huo alisema kampuni inaungana na familia na tasnia ya habari kutoa pole.

Wasifu wa Raymond

Raymond alizaliwa mwaka 1968 Iyunga mkoani Mbeya.

Raymond alipata elimu ya msingi wilayani Mufindi na baadaye alijiunga na sekondari ya Mpechi, Njombe mwaka 1986 hadi 1989.

Alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1996 katika kampuni ya The Guardian Limited.

Alijiunga na MCL mwaka 2012 na aliwahi kuwa mshindi wa pili wa tuzo za uandishi bora wa makala kuhusu watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Kabla ya uandishi wa habari, Raymond alifanya kazi akiwa mkutubi msaidizi katika Bodi ya Taifa ya Maktaba (TLSB), kwa miaka mitatu (1992 -1995).

Taaluma ya uandishi wa habari aliipata katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ mwaka 2007 hadi 2008 na kutunukiwa Stashahada.

Chanzo: mwananchi.co.tz