Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwandishi wa habari Dilunga afariki dunia

76108 Dilunga+pic

Tue, 17 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Jamhuri nchini Tanzania, Godfrey Dilunga amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne Septemba 17, 2019 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam,  alikokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Jamhuri  Media Limited, Deodatus Balile amesema Dilunga aliyezaliwa Oktoba 28, 1976 mkoani Morogoro alikuwa akisumbulia na maradhi ya tumbo na kabla ya kupelekwa Muhimbili alikuwa akitibiwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.

“Msiba umetokea leo saa 10 alfajiri kwa maradhi ya tumbo hasa typhoid ambayo ilikuwa sugu na alihamishiwa Muhimbili Septemba 9, 2019 hadi jana jioni tulikaa naye kabla ya kuhamishiwa ICU (chumba cha uangalizi maalumu).”

“Tulitoka jana usiku Muhimbili na alipewa huduma zote zilizotarajiwa kufikia, lakini kwa bahati mbaya leo asubuhi amefariki dunia. Hili ni pigo kwetu,” amesema Balile ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Hariri Tanzania (TEF).

Balile amesema wakati Dilunga akijiunga na Jamhuri Februari 1, 2019 alitokea gazeti la Raia Mwema na wao walianzisha mafunzo maalumu kwa ajili ya kumuweka kwenye mkondo wa habari za uchunguzi.

“Kwa kweli alikuwa ameiva kwa kiwango ambacho ungeweza kumuachia gazeti na ukaendelea na shughuli zako bila wasiwasi. Lakini wakati amekomaa na kuweza kusimamia habari za uchunguzi ametutoka ni pengo kubwa ametuachia kwenye kampuni,” amesema Balile.

Pia Soma

Advertisement
Amesema kwa sasa uongozi wa kampuni kwa kushirikiana na familia wapo katika mchakato wa kuandaa taratibu za kuaga mwili jijini Dar es Salaam kisha kusafirisha mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko.

Kwa mujibu wa Balile, Dilunga amewahi kufanya kazi katika magazeti ya Mtanzania, Raia Mwema kabla ya kujiunga na Jamhuri. Ameacha watoto watatu na mjane mmoja.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz