Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwananchi yaanda kambi ya afya D’Salaam

Fri, 5 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika kuendeleza juhudi za maisha bora, wadau wa afya wakishirikiana na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wameandaa kambi ya afya kesho jijini hapa, wakiahidi huduma za uhakika kwa wananchi watakaojitokeza.

Mratibu wa kambi ya afya ya Mwananchi, Naomi Kaale alisema jana kuwa maandalizi yaliyofanyika kwa miezi miwili yamekamilika na wapo tayari kuwahudumia wananchi watakaojitokeza kutambua afya zao kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni.

“Kila kitu kipo tayari. Kutakuwa na madaktari kutoka hospitali na kliniki pamoja na washauri nasaha. Watatoa vipimo vinayochukua muda mfupi kama vile vya presha au kisukari. Watakaobainika kuwa na matatizo makubwa watapewa rufaa kwenda kutibiwa hospitalini,” alisema Naomi.

Alisema kutakuwa na madaktari bingwa wa macho na meno pamoja na wa mazoezi ya viungo kwa wagonjwa (physiotherapy), “katika kurahisisha gharama, kampuni za bima ya afya zitakuwapo pia.”

Aleesha Adatia, daktari bingwa wa satarani wa Hospitali ya Aga Khan ambayo ni miongoni mwa taasisi zitakazokuwapo kesho, alisema watakuwa na timu kamili kuanzia wauguzi hadi madaktari ili kutoa vipimo na ushauri wa bure kwa watakaohudhuria.

“Tutakuwa na madaktari bingwa wa saratani na magonjwa ya wanawake na tutatoa vipimo vya saratani ya mlango wa kizazi na matiti bila malipo,” alisema Dk Aleesha.

Akizungumzia kambi hiyo, Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania, Dk Elizabeth Shekalaghe alisema, “nitoe wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi, elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa na haki na wajibu wa mgonjwa au mteja katika huduma za dawa zitaelezewa kwa kina,” alisema Dk Elizabeth.

Kwa miaka ya karibuni, vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza vimekuwa vikiongezeka kwa kasi. Wataalamu wanasema wengi hupoteza maisha kabla hawajajua tatizo kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kwenda hospitali kuchunguza afya zao au kushindwa kumudu gharama.

Kwa kuliona hilo, kampuni ya CRDB Insurance Broker inayotoa bima za aina tofauti ikiwamo ya afya itakutana na kuwasikiliza kasha kuwaelimisha wananchi watakaojitokeza kesho.

Mkurugenzi mkuu wa CRDB Insurance Broker, Arthur Mosha alisema anatamani wananchi wote wawe na afya bora ili kuchangia uzalishaji mali nchini.

“Kuwa na afya ni muhimu kuliko vitu vyote kwa binadamu, na ili Taifa liendelee tunahitaji watu wenye afya njema. Tumeshuhudia nchi ikipoteza nguvukazi kutokana na kukosa huduma bora za matibabu,” alisema Mosha.

Kusisitiza wananchi kujitokeza na kupima afya zao ili waanze utaratibu wa kutibiwa, Naomi alisema kutakuwa na wadau wengine wengi watakaoelimisha masuala ya lishe, huduma za fedha kwa wagonjwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na wananchi.



Chanzo: mwananchi.co.tz