Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Josephine Mngara (27), mkazi wa Mtemboni, Mji mdogo wa Himo, Mkoani Kilimanjaro anadaiwa kuuawa na mpenzi wake na kisha mwili wake kuchomwa moto.
Mwili huyo umekutwa kwenye pagale usiku wa kuamkia Februari 19 ukiwa umechomwa na kuteketea kwa moto ambapo mabaki ya mwili huo yamehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kwenye nyumba aliyokuwa akiishi marehemu na mume wake imekutwa michirizi ya damu kuelekea eneo ambalo mabaki ya mwili huo yamekutwa.
Amesema jeshi la polisi linaendela na uchunguzi wa tukio hilo.
"Kupitia Jeshi la Polisi kuna mambo mawili yanafanyika, kwanza kumtafuta mtu huyo ambaye nyumba yake imekutwa na michirizi ya damu mpaka eneo mwili ulipokutwa umeungulia," amesema
Aidha amesema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kitaalam ikiwemo kuchukua sampuli ya vinasaba (DNA) na kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kujiridhisha na tukio hilo.