Mwanamke aliyetambulika kwa jina la Joyce Masanja, anayekadiliwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35, mkazi wa Mtaa wa Kalonga Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia baada ya kuuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Januari 14, majira ya saa 6 usiku, ambapo mwanamke huyo amekutwa ameuwawa kando ya Msikiti wa Binti Haji uliopo Mtaa wa Kalonga Kata ya Ngokolo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, wanasema kuwa majira ya saa sita usiku walisikia sauti za mwanamke huyo akipiga kelele ya kuomba msaada, na baada ya muda mfupi, kelele hizo hazikusikika tena.
Baada ya kuamka alfajiri wakakuta mwili wa mwanamke huyo ukiwa umelala kando ya nyumba zilizoko karibu na Msikiti wa Binti haji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi amesema tayari jeshi hilo linamshikilia mtuhumiwa ambaye ni mume wa marehemu, kwa kuwa inaelezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanaume alimtuhumu mkewe kutoka kimapenzi na mwanaume mwingine.