Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanamke asimulia alivyopoteza watoto 15

17066 Watoto+pic TanzaniaWeb

Sat, 15 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanamke yeyote anapobeba ujauzito, matarajio yake ni kupata mtoto, lakini hilo limechelewa sana kwa Jenifer Peter aliyesota miaka 17 akitafuta mtoto bila mafanikio.

Licha ya mimba tano kuharibika na watoto 10 kuzaliwa kabla ya wakati wakiwa hai na baadaye kufariki dunia mbele ya macho yake, hakukata tamaa, aliendelea kujaribu bahati yake.

Jenifer (34) mkazi wa Kijiji cha Mwitende, Wilaya Bunda mkoani Mara sasa ana furaha isiyo na kifani baada ya kufanikiwa kumpata mtoto Neema kupitia huduma ya Kangaroo Mother Care (KMC) inayotolewa na madaktari waliopo kwenye mradi maalumu wa Martenal and Child Survival Program (MCSP) uliolenga kusaidia afya ya mama na mtoto.

Shughuli za mradi huo kwa sasa zinatekelezwa na mradi mpya wa USAID Boresha Afya yote ikifadhiliwa na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) na kutekelezwa na Jhpiego kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Haikuwa rahisi kwa Jenifer anayesema, “Niliolewa mwaka 2002 Kijiji cha Kiangasaga kwa mume wangu Samuel Nyamani, mimba ya kwanza ilitoka nyumbani ikiwa na miezi mitano, sikupata huduma yoyote.”

Anasimulia kuwa pamoja na mumewe waliendelea kujaribu, alibeba mimba ya pili ya tatu na nne, zote zilitoka na hapo alianza kupokea lawama kutoka kwa mama mkwe, ambaye alimweleza kuwa anahitaji wajukuu.

“Mama mkwe alisema ninawapa hasara, akaanza kumshawishi mume wangu aoe mke mwingine alinituhumu kuwa huenda nina magonjwa ya zinaa, wakanipa dawa nikanywa baadaye nikabeba mimba ikatoka tena, kelele zikazidi mume anataka kuoa mke mwingine, mara nina mashetani wakanipeleka kwa waganga wa kienyeji.”

“Niliendelea kubeba mimba na wakati huu zinatoka miezi sita au saba zingine nilikuwa nikijifungua lakini baada ya dakika chache watoto walikuwa wanafariki, mwaka 2009 mume wangu akaoa mke mwingine wakazaa watoto wawili, kwangu mimba 10 zikawa zimetoka, walisema nalazimisha uzazi kama imeshindikana niufunge, lakini shemeji yangu akaniambia nisifunge uzazi nitaendelea kutafutiwa matibabu.”

Jenifer anasema wakati mwingine mimba zilitoka nyumbani, “mtoto anafia chini, nikaenda Shirati wakaniambia mfuko wa uzazi umelegea, nikaja huku mama yangu mdogo akanipeleka hospitali wakashauri nifunge mfuko huenda mimba zitakua.”

“Walinifunga mfuko zikapita siku 3 mimba ikatoka, Novemba mwaka jana nilipobeba mimba hii nikaja hapa Mwitende ikiwa na miezi mitano, Januari 4, tumbo liliuma kwenda kuangalia nikaona damu, wakaanza huduma kufika saa 6, mimba ikatoka mtoto katoka akiwa hai.

“Waliniambia tutamuweka kwenye joto, asubuhi saa nne daktari alipitia akaniambia nitahamishwa na kuwekwa kwenye chumba changu mwenyewe wakanianzishia huduma ya Kangaroo, niliendelea kuishi kwa maelekezo kwa miezi mitatu wakaniruhusu kwenda nyumbani mtoto akiwa ameshakua.”

Hata hivyo Jenifer kwa majonzi mazito anasema mumewe anayeishi Shirati wilayani Rorya bado hajafika kumjulia hali yeye wala kumuona mtoto ambaye kwa sasa ana miezi mitano. “Japokuwa tunawasiliana hata asipokuja sina shida, ilimradi na mimi sasa naitwa Mama Neema.”

Anasema utofauti wa huduma katika hospitali zote na Kibara, mtoto alizaliwa hai kama ilivyo kwa wengine 10, lakini huduma aliyoipata imemwezesha kuokoa uhai wa binti yake.

Baba mdogo wa Jenifer, Joel Karangi anasema walikata tamaa baada ya mimba 15 za binti yao kutopata mtoto na kwamba ujauzito wa 16 walidhani pia ungetoka.

Anasema kama walivyohisi ilipofikisha miezi sita, bahati mbaya alipata tatizo la kutokwa na damu na walipompeleka Hospitali ya Kibara alipokewa kwa upendo na madaktari ambao walimhudumia kwa lengo la kumuokoa mtoto.

“Tulishtuka, wengine walitukatisha tamaa kabisa kwamba huyu mtoto hatakua, baadhi ya wahudumu wa hospitali walisema ni nadra kupona, lakini muuguzi mmoja anaitwa Vero alisema kwa mujibu wa mafunzo waliyoyapata mtoto atasalimika.”

Anasema hawakutegemea, kwani siku baada ya siku walipomtembelea waliona afya ya mtoto inazidi kuimarika.

Wasemavyo wataalamu

Afisa Muuguzi aliyemhudumia Jenifer katika Hospitali ya Kibara, Dominic Nyamima anasema walimpokea akiwa na ujauzito ambao waligundua ulikuwa na miezi sita na ulikuwa katika hatari ya kutoka.

Anasema walimpa mama huyo ushauri na kumweleza nini kinaendelea, baadaye alijifungua mtoto wa kike akiwa na gramu 750 ambapo kwa kawaida ni mtoto mdogo kulingana na umri wa mimba na uzito aliokuwa nao.

“Bahati nzuri mtoto aliendelea vizuri tukamwanzishia huduma zilizohitajika. tulimfundisha namna ya kumtunza mtoto kwa kutumia huduma ya Kangaroo ambapo ngozi ya mama na mtoto huwa zinakutana kwa ajili ya kumsaidia mtoto kupata joto la kutosha, kwani wanaozaliwa na uzito mdogo wanakuwa na athari ya kupunguza joto jingi na ndiyo chanzo cha kifo chao,” anasema Nyamima.

Anasema walikaa na Jenifer kwa miezi mitatu na baadaye walimruhusu kwenda nyumbani baada ya uzito wa Neema kufikia gramu 2500 sawa na kilo 2.5.

Nyamima anasema hayo ni mafanikio yaliyotokana na mafunzo maalumu kupitia mradi wa USAID Boresha Afya ambao uliwasaidia, kupitia mafunzo kazini na usimamizi mwingine ambao ni elekezi kazini.

“Kupitia elimu hiyo tumeweza kumwelekeza huyu mama katika kumkuza mtoto wake, ni elimu ambayo ilikuwepo lakini zamani tulikuwa hatuitumii vizuri.”

Nyamina anasema tukio la Jenifer hajawahi kukutana nalo katika muda wake wote aliofanya kazi hiyo. “Nimewahi kuhudumia mama ambaye amejifungua katika uzito mdogo wa gramu 1,500 na kuendelea kwangu ni kesi ya kwanza.”

Hata hivyo, anasema kulingana na uzito wa mtoto wa Jenifer, iwapo wasingekuwa wamepata mafunzo, ingekuwa vigumu kwao kuokoa maisha ya mtoto huyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Daktari wa kinywa na meno wa Mkoa Nilla Jackson, anasema kutokana na watumishi kujengewa uwezo katika huduma ya Kangaroo, wameweza kutoa huduma iliyo bora kwa Jenifer.

“Mradi umeboresha mafunzo kwa watumishi wetu ambao wamejengewa uwezo katika utunzaji wa watoto njiti kupitia mfumo wa ‘Kangaroo mother care’ tulipewa vifaa.

Dk Nilla anasema kumekuwepo na vifaa tiba na vitendanishi katika kuhakikisha huduma zinakwenda vizuri tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2014 katika mkoa wa Mara ambao umekuwa na matokeo chanya.

“Kwa sababu watumishi walijengewa uwezo na uliendelea kuwasaidia mpaka mwaka 2016 ulipoingia mradi wa USAID Boresha Afya, tangu hapo mpaka sasa vifo vimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Katika takwimu zilizopo kabla ya kuanza mradi mkoa ulikuwa na vifo 91, mwaka 2014 mradi ulipoanza vilishuka na kufikia 67, mwaka 2015 vikawa 65 na mwaka 2016/2017 vilifanana kwa namba 58, lakini Januari mpaka Juni mwaka huu Mkoa una vifo 21 pekee,” anasema Dk Nilla.

Dk Nilla anasema hiyo imewawezesha kujenga uwezo kwa watumishi wa afya na vituo vingi wigo wa upasuaji wa dharura umetanuka na kupunguza rufaa.

Anasema jitihada zingine ilikuwa ni kuhakikisha jamii katika ngazi za kaya kujua umuhimu wa kutumia vituo vya afya, kujifungua kituoni na huduma zingine pasipo kutumia mitishamba au wakunga wa jadi.

“Hilo tumefanikiwa, Mkoa wa Mara kwa sasa wanaume wameinuka zaidi wanajua umuhimu wa ushiriki wao katika kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaimarika na haya ndiyo yanasababisha huduma ya mama na mtoto iimarike.”

Akizungumzia mradi huo, Dk Nilla anasema USAID Boresha Afya umekuja kwa namna tofauti kwa kutoa mafunzo ya vituoni yenye uimara mkubwa na yamesaidia kupunguza kutokuwepo kwa wahudumu vituoni na wakufunzi wanapopita kutoa mafunzo wamekuwa wakisaidia kutoa huduma kwa vitendo ni mafunzo shirikishi.

Chanzo: mwananchi.co.tz