Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi mjamzito asimulia mkasa wake

26634 Pic+mjamzito TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Neema Shukurani, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisangura, Wilaya ya Serengeti anayedaiwa kupewa ujauzito na askari magereza, Yohana Tangawizi ameomba asihukumiwe bali asaidiwe.

Tangawizi aliyekuwa sajenti katika Gereza la Mradi Tabora B, alijiua Ijumaa iliyopita kwa kujipiga risasi mbili mdomoni akiwa nyumbani kwake. Kabla ya kujiua aliacha ujumbe kuwa amejiua kwa sababu ya kuumwa tumbo muda mrefu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndakin akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo alisema Tangawizi alikuwa amefunguliwa jalada katika Kituo cha Polisi akituhumiwa kumpa mimba mwanafunzi wa sekondari.

Jana, Mwananchi lilizungumza na Neema anayesoma kidato cha pili aliyekiri kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Tangawizi tangu Juni mwaka huu na walikuwa wanakutana vichakani kwa kuwa gereza linapakana na kijiji na pia shule yao.

“Alikuwa ananiahidi kunisaidia maana alikuwa ananipa fedha za matumizi shuleni elfu tano tano hizi, pia akawa anadai nisiwe na wasiwasi ataendelea kunisaidia sana, sasa sijui itakuwaje maana ameishakufa,” alisema mwanafunzi huyo kwa sauti yenye majonzi.

Alisema baada ya kupata ujauzito, alimtaarifu askari huyo kwa njia ya simu.

“Nilipompigia (simu) alidai nisiwe na wasiwasi, lakini akaomba tuonane ana kwa ana, mpaka suala hili linajulikana shuleni nilikuwa sijaonana naye ana kwa ana huenda alipata taarifa zilizomstua,” alisema.

Kuhusu ndoto zake alisema anataka kuwa muuguzi, lakini kwa hali ilivyo hajui hatima yake hivyo anaomba wazazi na jamii wasimhukumu bali wamsaidie.

Ghisango Mwita, mkuu wa shule anayosoma Neema alikiri kuwa huyo ni miongoni mwa wanafunzi wake waliotakiwa kufanya mtihani wa kidato cha pili kuanzia leo, lakini kwa sheria za shule akishabainika ana ujauzito haruhusiwi tena.

“Taarifa iko ngazi ya wilaya na tayari suala lake lilikuwa polisi, hivyo kwenye ngazi yetu huku sisi hatuhusiki tena.” alisema



Chanzo: mwananchi.co.tz