Sengerema. Ayoub Yahya (19), mwanafunzi wa kidato cha tano Shule ya Sekondari Sengerema wilayani Sengerema mkoani Mwanza anadaiwa kujinyonga hadi kufa kwa kutumia chandarua.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Advera Bulimba amesema tukio hilo limetokea Oktoba 18, saa 12 asubuhi.
Amesema mwanafunzi huyo mwenyeji wa Kyerwa mkoani Kagera alikutwa akining’inia kwenye mti uliopo pembeni ya uwanja wa mpira wa shule hiyo.
“Mwili wa mwanafunzi huyo ulibainika baada ya wanafunzi wenzake kupita karibu na uwanja huo kabla ya kutoa taarifa kwa uongozi wa shule ambao ulifikisha taarifa hizo kituo cha polisi,” amesema Bulimba.
Alisema chanzo cha mwanafunzi huyo kujinyonga bado hakijafahamika na kwamba mwili umehifadhiwa Hospitali ya DDH Sengerema kwa ajili ya uchunguzi.
Septemba 4, 2018 mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Rau mjini Moshi, Emmanuel Tarimo (18) alijinyonga hadi kufa baada ya kuhojiwa na jopo la walimu kuhusu tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi mwenzake.