Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi kidato cha sita afariki ghafla katikati ya mitihani

Mon, 13 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Songea. Wakati mitihani ya kuhitimu kidato cha sita ikiingia siku ya tano jana, mtahiniwa katika Shule ya Sekondari Kigonsera wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma, Khalifa Bakari (23) amefariki dunia baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye chumba mtihani.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma mchepuo wa Sayansi - Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) alifikwa na mauti juzi mchana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa alisema jana kuwa tukio hilo limetokea juzi saa saba mchana huko Kigonsera, Mbinga.

Alisema mwanafunzi huyo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Kigonsera baada ya kuzidiwa ghafla wakati akiwa kwenye chumba cha mtihani. Alisema taarifa za kidaktari zinaeleza kuwa marehemu alikua na upungufu wa damu na tatizo la kupumua.

Alisema hadi umauti unamfika, mwanafunzi huyo alikuwa ameshafanya mitihani ya General Study, Hisabati 1, Fizikia 1 na Kemia.

Mkuu wa shule hiyo, Ponsiano Ngunguru alisema mwili wa mwanafunzi huyo ulisafirishwa juzi saa tatu usiku kupelekwa nyumbani kwao Tanga mjini kwa mazishi.

Pia Soma

Alisema tukio hilo limeleta huzuni kubwa kwa wanafunzi wenzake na jamii inayozunguka shule hiyo.

Aliwataka wanafunzi kuwa na tabia ya kutoa taarifa pindi wanapokuwa na matatizo ya kiafya na wazazi wawatafutie bima za afya.

Mmachinga asakwa kwa kubaka

Katika hatua nyingine, polisi mkoani humo wanamsaka mfanyabiashara mdogo ‘mmachinga’ kwa madai ya kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa Mnazini wilayani Namtumbo na kumpa ujauzito ambao sasa umefikisha miezi saba.

Kamanda Maigwa alisema tukio hilo limetokea wakati binti huyo alipokwenda katika Soko la Namtumbo ambako alilaghaiwa na mchuuzi huyo na kufanya naye mapenzi vichakani na siku hiyohiyo akapata mimba.

Chanzo: mwananchi.co.tz