Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Ndugu, Mbozi mkoani Songwe, Daud Simkoko (17), ameuawa kwa kipigo kisha kuchomwa moto na wananchi kwa tuhuma za wizi katika duka la huduma za kifedha.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Rashid Ngonyani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuwa tayari kueleza kama Simkoko alikuwa mwanafunzi lakini taarifa za uhakika kutoka katika vyanzo mbalimbali zimethibitisha kuwa alikuwa mwanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda Ngonyani alisema tukio hilo lilitokea Machi 5, mwaka huu, majira ya saa 5:03 usiku katika eneo la Soko Kuu, mjini Vwawa, wilayani Mbozi.
"Mtuhumiwa (marehemu) alikamatwa na walinzi wa maduka kwa kushirikiana na wananchi akiwa ndani ya duka la miamala ya kifedha linalofahamika kama Kapamato akiwa amekata sehemu ya bati la paa la jengo hilo na kuingia ndani kwa lengo la kuiba," alisema.
Ngonyani alisema kijana huyo aligunduliwa na walinzi baada ya kuwakurupua wenzake wawili waliokuwa nje na ambao walikimbia na kumwacha akiwa ndani ya jengo.
"Walinzi baada ya kuona hivyo, walipuliza filimbi kwa lengo la kuomba msaada na mtuhumiwa alipojaribu kukimbia, walinzi kwa kushirikiana na wananchi waliojitokeza, walifanikiwa kumkamata na kuanza kumshambulia na kisha kumchoma moto," alisema Ngonyani.
Alisema polisi walipata taarifa na askari waliokuwa doria walipofika eneo la tukio, walikuta tayari mtuhumiwa huyo alikuwa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa Ngonyani, Simkoko baada ya kutoboa bati na kuingia ndani, aliharibu mfumo wa kamera ya mfumo wa ulinzi (CCTV) uliokuwa umefungwa ndani ya duka hilo.
Pia Kamanda Ngonyani alisema kabla ya tukio hilo, kijana huyo tayari alikuwa anatuhumiwa kwa matukio ya wizi kwa kutumia mbinu hiyo hiyo ya kutoboa bati na kuingia ndani.
Alisema Januari 18, mwaka huu, alikamatwa kwa wizi katika maduka matatu katika mtaa wa Ilembo, wilayani Mbozi na kuiba Sh. 2,358,000 na vitu vingine kama simu sita za mkononi na mafuta ya kupaka aina ya Family.
"Mtuhumiwa baada ya kuhojiwa, alikiri kutenda kosa hilo na kufikishwa mahakamani kwa kesi kumbukumbu namba JUV.01/2023 kosa kuvunja duka usiku na kuiba," alisema Ngonyani.
Uongozi wa Shule ya Sekondari ya Ndugu ulipoulizwa kuhusu mwanafunzi huyo, ulithibitisha kuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa kidato cha nne na kwamba tengu Januari, mwaka huu, hakuwa shuleni baada ya kushtakiwa mahakamani kwa madai ya wizi.
"Daud (marehemu) alikuwa mwanafunzi wetu na kwa mara ya mwisho aliripoti hapa Januari na baadaye akapata tatizo ambalo tulimsimamisha mpaka atakapolimaza na mwezi huu bodi ya shule ilitaraji kukutana na moja ya mambo ya kujadili lilikuwa suala lake.
Lakini katika mshangao mkubwa, tumepokea taarifa za kuuawa kwake," alisema mmoja wa viongozi wa shule aliyeomba jina lake lihifadhiwe.