Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa aomba haki itendeke

Mwanafunzi Ulawiti.png Mwanafunzi anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa aomba haki itendeke

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Masaunga wilayani Bunda (jina limehifadhiwa) anayedaiwa kubakwa na kulawitiwa, kisha kunyweshwa sumu na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Vicent Nkunguu, amewaomba kuharakishwa kwa hatua za kisheria ili haki ipatikane.

Mwalimu Nkunguu anadaiwa kufanya vitendo hivyo Machi 8 na 9, 2024 nyumbani kwake katika Kijiji cha Kisorya na inadaiwa alimnywesha sumu mwanafunzi huyo ili kupoteza ushahidi wa matukio hayo.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa katika hospitali teule ya Bunda leo Machi 15, 2024 mwanafunzi huyo amesema alishindwa kutoa taarifa juu ya tukio kutokana na kuona aibu pamoja na uoga.

"Nilikuwa naona aibu kwa kile kitendo alichonifanyia ndio maana hata nilipoonana na mama kesho yake nilishindwa jinsi ya kumwambia na pia nilikuwa naogopa, maana mwalimu alisema wazazi wangu wasijue.

Amesema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri, kwani anaweza kutembea, kuoga na hata kukaa tofauti na ilivyokuwa awali ingawa bado ana maumivu tumboni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amesema upelelezi juu ya tukio hilo unaendelea na upo katika hatua za mwisho.

"Kuna vitu tunavisubiri maana tumewashirikisha wenzetu wa ofisi ya mkemia mkuu, kwa hiyo vikikamilika tutapeleka jalada ofisi ya Taifa ya mashtaka kwa hatua zaidi," amesema.

Daktari wa wodi ya Wanawake katika hospitali Teule ya Bunda, Dk Chacha Philipo amesema mwanafunzi huyo hivi sasa anaendelea vizuri tofauti na alivyofikishwa hospitalini hapo Machi 11, 2024.

"Bado yupo hospitalini anaendelea na matibabu, lakini hali yake inaridhisha sio kama mwanzo," amesema Dk Philipo.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kufanyiwa vitendo hivyo Machi 8, 2024 alipokuwa amelala nyumbani kwa mtuhumiwa huyo alipokwenda kuwapikia watoto wa mtuhumiwa baada ya kuombwa na mke wa mwalimu huyo ambaye inadaiwa siku ya tukio alikwenda kwenye maombi katika Kijiji cha Igundu.

Machi 9, 2024 jioni mtuhumiwa huyo anadaiwa kunyweshwa sumu mwanafunzi huyo kwa lengo la kupoteza ushahidi, baada ya mwanafunzi kutaka kurudi kwa wazazi wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live