Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi aliyetoweka Mbeya apatikana

43815 Pic+mbeya Mwanafunzi aliyetoweka Mbeya apatikana

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi Mbeya kuonya kupotea kwa mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Lyoto, Aida Chaula (17), familia yake sasa imepata faraja baada ya binti huyo kupatikana.

Familia hiyo awali ilisambaza picha na kutoa namba za simu katika kijiwe cha bodaboda na bajaji cha Isyesye.

Akizungumza jana nje ya kituo kidogo cha polisi Ilomba jijini hapa alipokwenda kuhojiwa, Essau Chaula ambaye ni kaka wa mwanafunzi huyo alisema walilazimika kutumia mbinu hiyo kutokana na familia kugubikwa na simanzi ya kupotea kwa binti huyo.

“Licha ya kutoa taarifa polisi, kama familia tulilazimika kufanya kikao na kupanga mikakati ya kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha kupatikana kwake. Tulikubaliana kuchapisha picha na namba za simu na kisha kusambaza katika vituo vya bajaji na bodaboda ndani na nje ya Jiji la Mbeya,” alisema Chaula.

Alisema akiwa katika majukumu yake alipigiwa simu na vijana wa bodaboda wakimueleza kuwa mwanafunzi huyo ameonekana stendi ya bajaji Isyesye, walimfuatilia na kumkamata, lakini kijana aliyekuwa naye alikimbia.

“Pia, taarifa zilizotolewa kwenye gazeti lenu (Mwananchi) zimesaidia, kweli tumeona nguvu ya vyombo vya habari, tunashukuru sana na tunaomba mkawe chachu ya kuibua changamoto zinazoikabili jamii,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi jana, mama wa mwanafunzi huyo, Ester Chaula alisema anamshukuru Mungu kwa kupatikana kwa binti yake kwa sababu walikuwa hawalali wala kula bali ni kumuomba Mungu atende ukuu wake apatikane akiwa hai na ametenda.

“Tulikuwa hatulali, tulikosa amani, binti alikuwa anaishi kwa kaka yake, kama unavyojua kila mmoja anaongea lake,’’ alisema huku akishukuru kupatikana kwa mtoto huyo ingawa Kamanda wa Polisi Mbeya Urlich Matei hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz