Mwanafuzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Gibaso iliyopo wilayani Tarime mkoani Mara, amefariki dunia kwa kutumbukia kwenye shimo wakati akichota maji katika shimo lililochimbwa kwa ajili ya ujenzi wa choo katika kituo cha afya Gibaso.
Mashuhuda wa tukio hilo wanadai kuwa mwanafunzi huyo aliagizwa na mwalimu kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya walimu huku wakilalamikia tabia ya kuwafanyisha kazi ngumu wanafunzi hao ikiwemo kuchota maji na kulima shambani jambo ambalo limekuwa sugu katika shule hiyo.
Aidha, wananchi hao wamesema kuwa baada ya tukio hilo kutokea wamefanya jitihada za kuwatafuta walimu lakini walimu wa shule hiyo hawakuonesha ushirikiano na wanapoulizwa hudai kuwa mwanafunzi huyo ametoka kwao akiwa mgonjwa huku mashuhuda wa tukio hilo wakithibitisha merehemu kutumbukia kwenye shimo hilo la choo.
Aidha wazazi wa marehemu wamesema kuwa hawatakuwa tayari kama ukoo kuzika mwili wa marehemu iwapo walimu hao hawatashiriki katika msiba kwani wamekuwa wakiwatumia wanafunzi kufanya kazi za shamba mara kwa mara na kurejea nyumbani wakiwa wamechoka jambo aambalo limepelekea baadhi ya wanafunzi kuchukia masomo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Gibaso Chacha Wambura ameeleza kuwa mwanafunzi huyo amefariki akiwa shuleni na hatua mbalimbali zinaendelea ikiwemo kutatua mgogoro uliopo kati ya wazazi wa marehemu, wananchi na walimu ili mwili wa marehemu uweze kuzikwa na hatua mbalimbali za kisheria ziweze kuendelea.
Tayari watuhumiwa wanashikiliwa na jeshi la polisi kituo kidogo cha Gibaso na Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya Gibaso ambapo Mganga mkuu wa kituo cha afya Gibaso amegoma kuzungumza na vyombo vya habari huku akidai kuwa mpaka apate kibali kutoka juu.