Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanafunzi afariki akitekeleza adhabu shuleni

Mwanafunzi Adhabu Y Mwanafunzi afariki akitekeleza adhabu shuleni

Fri, 17 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwinuko iliyoko Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, Glory Faustine (14) amefariki huku mwingine, Emmanuel Lyatuu (13) akivunjika mguu wa kulia baada ya kudondokewa na jiwe wakitekeleza adhabu ya kuchimba kifusi.

Akizungumza leo Machi 17, 2023 Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema wanafunzi hao ni kati ya wanafunzi 30 waliokuwa wamepewa adhabu ya kusomba kifusi kama adhabu ya kuzungumza Kiswahili shuleni hapo.

Pia alisema jeshi hilo linamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalu Baluya (51) na Mwalimu wa zamu, Theonest Malosha (35) kwa tuhuma za kufanya uzembe uliosababisha madhara kwa wanafunzi hao.

"Wanafunzi 30 wa madarasa tofauti walipewa adhabu kuanzia jana (juzi) ya kusomba kifusi kwa ajili ya kufukia mitaro inayopitisha maji shuleni.

“Hii ni baada ya kukutwa wakizungumza lugha ya Kiswahili shuleni tofauti na ulivyo utaratibu wa shule unaowataka wazungumze lugha ya Kingereza wanapokuwa mazingira ya shuleni," alisema Mutafungwa

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mwanza, Mkaguzi wa Polisi, Kamila Laban amesema mwanafunzi huyo alifariki muda mfupi baada ya kudondokewa jiwe hilo.

"Mbali na tukio hili, niwatake wakazi wa maeneo ya milimani kuongeza ulinzi kwa watoto wao hasa wakati huu ambao mvua zinaendelea kunyesha kwa sababu zinasababisha udongo kupoteza uhimilivu na kusababisha mawe kuporomoka kwa urahisi," amesema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekouture, Dk Bahati Msaky akizungumza na Mwananchi kwa simu amesema mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo huku majeruhi watano kati ya sita waliopokelewa wakiruhusiwa baada ya afya zao kuimarika.

Amesema mwanafunzi aliyevunjika mguu wa kulia anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo huku watano wakiruhusiwa kutoka baada ya hali zao kutengemaa.

"Huyu ambaye mguu wake umevunjika tumeshamfunga bandeji (POP), wengine tumeshawapatia matibabu na kuwaruhusu kutoka hospitalini kwa sababu hawakupata madhara makubwa ikilinganishwa na hawa wengine," alisema Dk Msaki

Baba wa marehemu ambaye ni mkazi wa Mwinuko wilayani Ilemela mkoani hapa, Felician Makutano amesema, anakumbuka kauli ya mwisho ya mwanaye ilikuwa ni salamu wakati anaondoka asubuhi.

"Baba Shikamoo, naenda shuleni," amesema.

Anasema baada ya kusalimiana binti yake alimpatia fedha ya nauli na matumizi shuleni huku akipokea simu baada ya aaa mbili kupita kutoka dereva bodaboda (jina linahifadhiwa) akimtaka kufika shuleni kwani binti yake amepata ajali ya kudondokewa jiwe.

"Huyo bodaboda alinipigia simu akaniambia mtoto wangu amepatwa tatizo la kudondokewa jiwe amefariki ndiyo nikaja shuleni nimefika nikakuta mwili wake umeshanasuliwa kwenye jiwe lililomdondokea," alisema huku akisema taratibu za mazishi zitafanyika baada ya uchunguzi wa mwili unaofanywa Polisi kukamilika.

Akizungumzia adhabu hiyo, Mkazi wa Kishiri jijini Mwanza, Mary Nyanzagi amelitaka Jeshi la Polisi kufuatilia kwa karibu adhabu zinazotolewa na walimu kwa wanafunzi kabla hazileta madhara.

"Ninachoelewa ni kwamba adhabu kwa wanafunzi zinatolewa kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa kuzitoa umewekwa sasa nashangaa kuona mwanafunzi anapewa adhabu ya kusomba kifusi ili hali mwalimu anajua mazingira anayoenda kuchimba kifusi hicho siyo salama," amesema Nyanzagi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live