Mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) wa Shule ya Uuguzi na Afya ya umma (SoNPH) Ezekiel Sostenes amelazwa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kati Benjamin Mkapa baada ya kujirusha ghorofani.
Awali kabla ya tukio hilo juzi, kulikuwa na ujumbe wa WhatsApp ambao Mwananchi imeuona, uliosambaa mitandaoni ukionyesha majibizano kati ya mwanafunzi huyo akimlalamikia mkufunzi wake kuwa alimfelisha kwa makusudi.
Akizungumza jana Desemba 15, 2022 Dk Winnie Msangi kutoka hospitalini hapo amesema walimpokea mwanafunzi huyo jana akiwa kwenye hali mbaya.
Winnie amesema Ezekiel anaendelea na matibabu baada ya kupata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
"Tulimpokea jana na kufanyiwa huduma ya kwanza kwa sababu alikuwa kwenye hali mbaya ya maumivu, mpaka sasa majeraha makubwa tuliyoyabaini ni kwenye uti wa mgongo lakini anaendelea ja matibabu zaidi," amesema Daktari huyo.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo Ofisa habari wa Chuo cha UDOM, Beatrice Mtenga amedai kuwa hana taarifa za tukio hilo na kuomba kupewa muda wa kulifuatilia.