Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MwanaFA kuitoa Muheza kwenye changamoto hadi fursa

Muheza Pic Data MwanaFA kuitoa Muheza kwenye changamoto hadi fursa

Mon, 29 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mbunge wa Muheza mkoani Tanga, Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA amesema ndani ya miaka mitano ijayo anakwenda kuibadilisha Wilaya ya Muheza kutoka kwenye changamoto na kuwa fursa.

MwanaFA ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vinne vilivyopo kata ya Magila wilayani Muheza.

Amesema kuwa katika kipindi hicho kwa kushirikiana na viongozi wengine pamoja na Serikali watakwenda kutatua changamoto nyingi zinazowakabili wakazi wa Muheza tofauti na miaka ya nyuma.

Mwana FA amesema kuwa wilaya ya Muheza ina changamoto nyingi lakini tangu amechaguliwa miezi nane ameweza kufanya makubwa ya kimaendeleo kwa kushirikiana na Serikali huku akiahidi kuwa ndani ya miaka mitano ijayo watarajie mengi mazuri zaidi.

"Maendeleo makubwa yanakuja katika kipindi hiki ambacho mimi ni mbunge wenu, kauli hii naweza kuitetea sehemu yoyote sababu vituo vya afya vitaongezeka, zahanati zitaongezeka shule zitajengwa na kuongezeka na barabara zitajengwa" amesema.

Amesema mwaka 2015 hadi 2020 Muheza walijenga madarasa 20 lakini katika kipindi cha miezi nane ambacho amekaa kuwenye nafasi hiyo tayari wameshajenga madarasa 63 na sasa Serikali imewapatia madarasa 67 hivyo kufikia jumla ya madarasa 130.

Wananchi wa vijiji hivyo wameahidi kumpa ushirikiano mbunge wao ili aweze kutimiza aliyoyaahidi wakati wa kampeni na wakati anapopita kuwashukuru wapiga kura wake.

"Sisi tunakupa mtihani huu wa kutatua changamoto zetu na kama endapo utashindwa kututimizia tunaomba mwaka 2025 usije kutuomba kura" amesema Peter Maua.

Mbunge huyo Yuko katika ziara ya kupita vijiji kwa vijiji lengo kukagua miradi ya maendeleo na kutoa shukrani kwa wapiga kura wake waliomchagua kuwa mwakilishi wao.

Chanzo: mwananchidigital