Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwamuzi adakwa na Takukuru kwa rushwa ya Sh120,000

44298 Takukuru+pic Mwamuzi adakwa na Takukuru kwa rushwa ya Sh120,000

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro, inamshikilia mwamuzi wa kati wa mpira wa miguu, kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh120,000.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 28, 2019 na mkuu wa Takukuru mkoa Kilimanjaro, Holle Makungu, imemtaja mwamuzi huyo kuwa ni Safiel Elias Mjema ambaye ni maarufu kwa jina la "Machachari".

Holle amesema Machachari alikuwa amepangwa kuwa mwamuzi wa kati katika mechi ya kutafuta bingwa wa mkoa wa Kilimanjaro, kati ya timu ya New Generation na timu ya Familia.

Inadaiwa baada ya kupata nafasi hiyo, mtuhumiwa huyo anadaiwa kumtumia ujumbe wa simu, mmoja wa viongozi wa timu shiriki akimjulisha kuwa yeye ndiye atakuwa mwamuzi wa kati.

Katika ujumbe huo, Holle alidai mwamuzi huyo anadaiwa alimtaka kiongozi huyo ampe Sh120,000 ili awape upendeleo kwenye mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa CCM Bomang'ombe wilaya ya Hai.

"Viongozi wa timu hiyo hawakuridhishwa na madai hayo hivyo walitoa taarifa Takukuru na mtego uliandaliwa na kufanikisha kumnasa mwamuzi huyo akiwa amepokea fedha hizo za mtego wa rushwa," alidai Holle.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Takukuru, mwamuzi huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zake mara tu uchunguzi wa tuhuma dhidi yake utakapokamilika.

Katika huo mchezo timu zilitoka hizo bila kufungana lakini New Generation ndio mabingwa wa mkoa wa Kilimanjaro baada ya kufikisha pointi 31 na Familia ikiwa na pointi 30.

 

Mwisho



Chanzo: mwananchi.co.tz