Mwalimu mkuu wa shule moja wilayani Bunda Mkoa wa Mara anashikiliwa na polisi akidaiwa kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali teule ya wilaya hiyo.
Mbali na kubakwa na kulawitiwa, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16, anadaiwa kunyweshwa sumu na mwalimu huyo kwa lengo la kupoteza ushahidi. Tukio hilo limetokea nyumbani kwa mtuhumiwa huyo Machi 9, mwaka huu.
Akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo alidai siku hiyo binti huyo hakurudi nyumbani, badala yake alibaki kwa mwalimu huyo kwa ajili ya kuwapikia watoto wake.
“Mke wa mwalimu ni ndugu yetu, siku hiyo alimuomba mwanangu abaki kwake, ili awapikie watoto wake kwa kuwa yeye anakwenda kwenye maombi, sisi tulipojulishwa hatukuwa na wasiwasi.
“Kabla ya siku hiyo, siku zote mtoto wangu huwa harudi nyumbani mchana, anakwenda kwa mwalimu kuwapikia watoto kwa sababu mke wa mwalimu aliomba iwe hivyo kwa sababu yeye ni fundi cherehani. Tulikubali ombi lake na mtoto hakuwahi kusema kama kuna shida yoyote,” alieleza.
Alidai siku hiyo saa 3 usiku alipigiwa simu na mpangaji mwenzake kuwa binti yake yupo katika maeneo yao na hali yake si nzuri, lakini alimjibu kuwa binti yupo nyumbani kwa mwalimu mkuu na hawezi kuwa katika maeneo hayo kwa muda huo.
“Baada ya muda mwanangu mkubwa akanipiga simu kuwa mtoto ameokotwa jirani na nyumbani kwake akiwa na hali mbaya, hii ni baada ya hao majirani kumpigia simu kwa sababu muda huo hakuwepo nyumbani kwake na alipofika akamtambua mdogo wake na kutujulisha," alifafanua.
Alieleza akiwa kituo cha afya siku ya Jumapili, mtuhumiwa alifika akiwa ameongozana na mkewe na binti yake alipowaona alijifunika shuka usoni, akawa hataki kuwaona wala kuzungumza nao.
Baadaye mtuhumiwa huyo alimpigia mama huyo simu na kumuomba suala hilo alifanye kuwa siri kati yao na amshawishi mtoto asitoe tuhuma hizo za ubakaji.
Mbali na simu, mama huyo alieleza kuwa mtuhumiwa alimtumia ujumbe mfupi wa maneno mara nne akisisitiza suala hilo liwe siri.
“Hadi sasa hatujui mtoto alifikaje katika eneo lile akiwa katika hali ile, kwa sababu alikuwa nyumbani kwa mwalimu, na mbali na vipimo vya hospitalini mimi pia nimemkagua mwanangu ni kweli ameingiliwa mbele na nyuma ...pia anatoa harufu kali,"
"Mwanangu kuna muda hajitambui, nadhani amepata shida ya kisaikolojia, hapo alipo hawezi kukaa wala kutembea, chakula pia anashindwa kula vizuri, namshukuru DC tangu jana alivyoingilia kati suala hili,” alisema
Daktari wa wodi ya wanawake katika hospitali Teule ya Bunda, Dk Chacha Philipo alisema vipimo vya awali vilionyesha michubuko sehemu za siri za mtoto huyo na uchunguzi zaidi unatarajiwa kufanyika baadaye leo.
Mwananchi lilifka hospitalini alipolazwa mwanafunzi huyo na kushuhudia akizungumza mambo yasiyoelewaka na pia alikuwa akitoa harufu kali iliyoelezwa kuwa ni sumu ya kupuliza kwenye mimea na kulalamika tumbo kumuuma.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano alikiri kutokea taarifa ya tukio hilo na kusema mwalimu huyo anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.
Alisema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo alikwenda kituo cha afya Kisorya alipolazwa mwanafunzi huyo na kutokana na hali yake kutokuwa nzuri aliagiza apewe rufaa kwenda hospitali hiyo teule.