Utata umeibuka kuhusu kifo cha mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari iliyoko Pasua, Manispaa ya Moshi, Walter Ebenezer, anayedaiwa kushambuliwa kwa mateke kwenye mbavu na mwalimu wake kisha kupewa adhabu ya kupiga ‘push up’.
Kutokana na kifo hicho, ndugu wa mwanafunzi huyo wamejitokeza hadharani wakiliomba Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kufanya uchunguzi wa kitabibu kubaini sababu za kifo hicho.
Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo kabla ya kupoteza maisha Februari 19 mwaka huu kwenye Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) alikokuwa anapatiwa matibabu, alikuwa mwanafunzi wa bweni wa shule hiyo.
Akizungumzia tukio hilo jana, mama mdogo wa marehemu, Mkazi wa Sakina-Arusha, aliyejitambulisha kwa jina moja la Neema, alidai kuwa kabla mwanafunzi huyo hajafariki dunia, aliwaambia kwamba alipigwa na mwalimu wake mateke kwenye mbavu na aliambiwa apige push up kutokana na kosa ambalo hakuliweka wazi.
"Baba mzazi wa marehemu, alipigiwa simu akaambiwa akamchukue mtoto maana anaumwa sana. Alipokwenda shuleni kumchukua mtoto, alimleta Mount Meru kwa ajili ya matibabu.
"Alipofikishwa Mount Meru, alipatiwa matibabu na aliwekewa oksijeni. Baadaye mtoto alipoteza maisha. Lakini tulikwenda kufuatilia polisi. Tulianzia Central Arusha (Kituo Kikuu cha Polisi) na baadaye tukaelekezwa twende Central ya Moshi mahali ambako tukio ndiko lilitokea.
"Tulimwelezea OCD Moshi (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) tukio zima na akachukua gari na askari na wakaenda shuleni, hawakumpata mwalimu, wakaambiwa warudi siku iliyofuata.
"Niliwauliza polisi kama tunaruhusiwa kuuzika mwili, nikaambiwa 'hapana!', tunatakiwa kusubiri mpaka wafanye uchunguzi wao," alidai.
Hata hivyo, mama mdogo wa mwanafunzi huyo aliendelea kudai kuwa walipokwenda Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, waliambiwa wanatakiwa wauzike mwili huo.
"Tunashangaa tutazikaje wakati Central Moshi wametuzuia na ndio ambako tukio limetokea? Tunazikaje huo mwili, mbona wanafamilia tunachanganywa? Tunazikaje wakati hatujajua mwafaka wa ndugu yetu amekufakufaje? Tunahitaji haki, uchunguzi ufanyike," alisisitiza.
Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi (ACP) Simon Maigwa, alikiri jeshi hilo linamshikilia mmoja wa walimu wa shule hiyo (hakumtaja jina) kwa ajili ya uchunguzi.
"Tumefungua jalada la uchunguzi. Kwa sababu ni malalamiko, ni jukumu letu kumshikilia ili tujiridhishe. Timu yangu ya makachero imekwenda kufanya postmortem (uchunguzi wa kitabibu) ili tujiridhishe kwamba ni kweli aliuawa au alikuwa anaumwa?
"Tunachunguza lakini hatuwezi kusema moja kwa moja. Sasa kumshikilia ni jukumu letu, kwa sababu kuna malalamiko juu yake. Tunasubiri madaktari, watuambie kwamba chanzo cha kifo chake ni nini.
"Makachero wetu wamekwenda huko (Hospitali ya Mount Meru) kujiridhisha kwanza na hiyo taarifa, kama kweli ipo na kama ipo, basi washirikiane na ndugu ili 'ku-clear' (kumaliza) hiyo doubt (shaka). Bado uchunguzi unaendelea, tunamshikilia kwa ajili ya uchunguzi na sio kwa sababu ya mauaji," alisema.