Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu auawa na kuporwa pikipiki

488b015aeeba1c92994e60995101c646.jpeg Mwalimu auawa na kuporwa pikipiki

Sat, 11 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwalimu wa Shule ya Msingi Busambara wilayani Musoma, Dickson James (27), ameuawa na kuibiwa pikipiki yenye namba za usajili MC 179 CYQ, aina ya Super Tiger.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishubwamu alisema jana kwamba Desemba 7, mwaka huu, saa 2:00 usiku katika Kitongoji cha Nyakato, Kijiji cha Nyang’oma mwili wa mwalimu huyo ulikutwa ukiwa umetelekezwa mashambani huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa kamba.

“Tunawashikilia watu wawili kuhusiana na tukio hili na uchunguzi bado unaendelea,” alisema RPC Tibishubwamu bila kuwataja majina.

Katika hatua nyingine, alisema watuhumiwa 22 wanashikiliwa na jeshi hilo kwa makosa mbalimbali baada ya operesheni maalumu ya kufunga mwaka iliyoanza Oktoba 26 hadi Desemba 9, mwaka huu katika halmashauri zote za mkoa huo kwenye maeneo ya majini na nchi kavu.

Alitaja mali za wizi zilizokamatwa kuwa ni pikipiki 12, magodoro 11 likiwemo moja la Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kwangwa, redio nane za aina tofauti na jenereta moja.

Mali nyingine ni televisheni 14, simu janja aina tofauti sita, kompyuta mpakato tatu, ndoo za rangi mbili, mitungi ya gesi sita, vichwa vya cherehani viwili na mashine za kusukumia maji mbili.

Pamoja na hayo, alisema walibaini stoo bubu iliyokuwa ikitumiwa kuhifadhi mali za wizi, katika Mtaa wa Nyakato Mlimani, Manispaa ya Musoma na ilipopekuliwa kulikutwa viti vya plastiki 46 na keni tano mali ya Kiwanda cha Maziwa cha Musoma Diary.

Vingine vilitajwa kuwa ni saruji mifuko 32, mabati 32, mizani mitatu, nondo zenye ukubwa tofauti na mota moja.

Alisema pia wanawashikilia watu 12 ambao walikutwa na nyara za serikali ambazo ni vipande 23 vya wanyama pori.

Kwa mujibu wa RPC huyo, walikamata lita 140 za pombe aina ya gongo pamoja na mtambo mmoja wa kuitengeneza ambapo jumla ya watuhumiwa 13 wanashikiliwa na polisi.

Alisema pia kuwa watuhumiwa watatu wanashikiliwa kwa makosa ya kukutwa na bangi ambapo jumla ya misokoto 960 na kilo nane za bangi zilikamatwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live