Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu amwokoa mwanafunzi na mapenzi ya jinsia moja

Mwee (21).jpeg Mwalimu amwokoa mwanafunzi na mapenzi ya jinsia moja

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwalimu Happyness Muro, mkazi wa Kibosho, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, amepewa 'kongole' na viongozi wa serikali za vijiji na wanaharakati, baada ya kufanikiwa kumwokoa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika eneo hilo, aliyekuwa ameanza kushiriki mapenzi ya jinsia moja ya usagaji.

Mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa), alikuwa akifanyiwa ukatili huo wa kingono na dada zake, ambao ni watoto wa mama mdogo.

Mwalimu Muro, alitoa ushuhuda huo wakati wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo viongozi wa serikali ngazi ya vijiji, wanaonolewa na Shirika la kiraia la KWIECO, linalofadhiliwa wa Women Fund Tanzania Trust (WFT Trust), kupitia mradi wa jitihada za jamii katika kuzuia na kutoa taarifa dhidi ya wanawake na watoto.

Mwanafunzi huyo anayedaiwa kuanza usagaji akiwa darasa la tano, ni kati ya wanafunzi 20 waliookolewa na Mwalimu Muro, kwenye matukio ya ukatili wa kijinsia katika Kata ya Kibosho Magharibi.

“Nimeokoa watoto wengi kwenye ukatili, mmoja ni mwanafunzi ambaye mama yake mzazi, alikuwa na watoto wengi wa kiume na huyo mmoja wa kike.

“Ili kumlinda mwanawe asiharibiwe, alimpeleka kulala kwa mama yake mdogo, ambako alikuwa analala na dada zake watoto wa mama mdogo. Wakati huo alikuwa darasa la tano; dada zake hao wakawa wanamfanyia usagaji (ukatili wa kingono).

“Sasa alipofika kidato cha pili, siku moja alienda kutembea mtaani, akachelewa kurudi nyumbani, akajua akienda kwa mama mdogo kulala atachapwa.

…Ikabidi aende kwa bibi akalala, kesho yake akarudi kwa mama mdogo akaja shuleni. Mama akaja shule kuripoti na kudai huyo mtoto ameanza tabia sio nzuri na walimu wakaanza kumchapa.”

“Wakati anachapwa, mimi natokea darasani nikakuta wanamchapa na kumhoji ili atoe majibu sahihi, nikawaambia mwacheni niwasaidie. Nilikaa na huyo mwanafunzi tukaongea kirafiki, nikamwambia utoe kwenye moyo wako wadhifa wangu kama mwalimu, tuongee mimi na wewe kama dada yako.

“Nikamuuliza ilikuwaje hebu nieleze, akaniambia mimi nililala kwa bibi ila nina kero yangu naomba usimwambie mama. Mimi nalala na dada zangu wa mama mdogo ila nataka niwakwepe kwa sababu wananisaga.”

Baada ya kugundua shida ya mwanafunzi huyo, alirejea kuwaeleza walimu wenzake kwamba msichana huyo hakulala na rafiki wa kiume, isipokuwa alikimbia kitendo cha kusagwa.

Redempta Tarimo, amempongeza Muro kwa ujasiri wake na namna alivyoamua kumnasua na kubadili maisha ya mwanafunzi huyo.

Katika kikao kazi hicho kilichowashirikisha mabalozi wa nyumba 10 na wanaharakati kutoka vijiji vya Uchira, Karamsingi, Lole na Kibosho, mratibu wa mradi wa jitihada za jamii katika kuzuia na kutoa taarifa dhidi ya wanawake na watoto, Veronica Ollomi, alisema lengo la kikao hicho ni kujengeana uwezo wa kuimarisha jitihada za wananchi na viongozi wao, kutafuta suluhu ya matatizo ya ukatili wa kijinsia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live