Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu aliyejipatia umaarufu kwa kucheza na wanafunzi wake

61008 Mwalim+pic

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii hususan Instagram, wiki iliyopita miongoni mwa video zilizozunguka sana ni za mwalimu anayeonekana akicheza na wanafunzi wake.

Mwalimu huyu kwa umri anaonekana kuwa ni binti mdogo lakini namna anavyofanya kazi yake kwa moyo amejijengea taswira ya aina yake. Utofauti huo ndio umemfanya kuwa kivutio mitandaoni na kugusa hisia za watu wengi kutokana na namna anavyotekeleza wajibu wake.

Kupitia akaunti yake mwandishi wa makala haya alimtafuta na kumfuata hadi shuleni anapofundisha ili kujua ukweli wa kinachoonekana mitandaoni.

Anafunga safari hadi Tabata Chang’ombe kuitafuta shule anayofundisha ya Patmo Junior School na anapowasili anapokelewa na kelele za wanafunzi wakiimba. Anapochungulia kwenye darasa hilo yupo mwalimu

Mwalimu huyo ni Joyce Kiango, alikuwa katikati ya watoto hao wakiimba na kucheza kwa kuzitaja herufi, tarakimu, viungo vya mwili na rangi.

Uso wake ukiwa umejawa tabasamu mwalimu Kiango anajichanganya na watoto hao kana kwamba naye ni wa rika lao na baada ya dakika kadhaa anamaliza na tunaanza kuzungumza.

Pia Soma

“Huwa najisikia raha sana ninapokuwa na watoto, nikiwaangalia nawaona kama wanangu, marafiki na watu wangu wa karibu zaidi. Huenda ni kwasababu nilipoteza mama nikiwa mdogo ndio sababu nataka watoto wapate upendo.”

Hivyo ndivyo anavyoanza binti huyo wa miaka 25 akijitambulisha kuwa ni mwalimu wa wanafunzi kuanzia miaka minne hadi sita. Kazi hiyo aliianza akiwa na miaka 21, muda mfupi baada ya kumaliza masomo yake ya ualimu.

Anasema licha ya kuwa tangu akiwa mdogo alitamani siku moja awe mwalimu lakini mapenzi yake kwa watoto ndiyo yamemfanya kuonekana ni mwalimu wa tofauti.

“Tangu nikiwa mdogo nikiulizwa Joyce ukiwa mkubwa unataka kuwa nani siku zote chaguo langu lilikuwa ualimu, sikufahamu wa ngazi gani ila nilitamani kufundisha,”

“Nilipomaliza kidato cha nne, nikaomba anipelekwe chuo cha ualimu na nikavutiwa kujifunza kuwa mwalimu wa watoto wadogo, ndipo safari yangu ya ualimu ilipoanza,”

Anasema akiwa chuoni alifunzwa kuwa na ubunifu katika ufundishaji na alipoanza kazi hilo alilipa kipaumbele katika kuhakikisha watoto anaowafundisha wanaelewa.

Alifikaje mitandaoni

Joyce anasema kuwa alibaini kuwa kundi la walimu wa chekechea limekuwa nyuma na hata walimu wenyewe wengi hawajivunii kazi hiyo.

“Nilikaa nikajiuliza hivi kwa nini walimu wa chekechea hawafahamiki, yaani tupo wengi lakini ni kundi ambalo lipo nyuma, hatujitambulishi kwenye jamii. Unakuta mtu hayuko radhi kutamka hadharani kuwa yeye ni mwalimu wa chekechea, nilitamani kubadilisha hilo na nikaona nianze mimi,”

“Nikawaeleza viongozi wangu wa shule na kwa kuwa nia yangu ni njema walinielewa na kuniruhusu niwe napost video fupi nikiwa na wanafunzi wangu darasani.”

Video hizo ndizo zilisambaa mitandaoni na kumpa umaarufu Joyce huku kila kukicha akiongeza idadi ya watu wanaofuata kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Anachokifanya mwalimu huyu ni kutumia ngoma na muziki katika ufundishaji wake, ndani ya nyimbo na burudani hiyo kunakuwa na yale anayotakiwa kufundishwa mwanafunzi wa elimu ya awali.

Cha ziada anachofanya ni kujifunza kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo vitabu, video za youtube na mafunzo na semina anazohudhuria mara kwa mara.

Hilo linaungwa mkono na mwalimu mkuu wa shule hiyo Charles Malango anayemsifia Joyce kwa ubunifu na umahiri wa kuwa karibu na wanafunzi.

“Kiukweli mwalimu huyu ni mbunifu, ukiamuangalia alivyo msichana mdogo unaweza usiamini kama anaweza kuwa karibu na watoto kiasi hiki baada ya kutumia muda wake kwa ajili ya mambo yake binafsi,

“Hajataka ujana wake abaki nao mwenyewe, ameamua ku-share anavyovijua na kuvileta katika masomo ya watoto na kwa kuwa hafanyi kitu kibaya tumemruhusu na binafsi nakuwa naye kumpa mwongozo pale ninapoona kidogo anazidisha,”

Malango anasema Joyce wa sasa si aliyempokea miaka minne iliyopita wakati anajiunga na shule hiyo, kujifunza kwake kumemfanya kuwa mwalimu wa aina yake.

Mara kadhaa anakuwa na mawazo na kuyapeleka kwenye uongozi wa shule kwa utekelezaji na yamekuwa yakifanyiwa kazi.

Malango anakiri kuwa Joyce amekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya wanafunzi wa shule hiyo maana wazazi wengi wamekuwa wakivutiwa na mtindo wake wa ufundishaji na wamekuwa wakimfuatilia kupitia mitandao.

“Tangu mwaka jana tumekuwa tukiona mchango wake, watoto wameletwa wengi na wazazi wanaonekana kumfurahia mno, tunachokifanya ni kumpa nafasi afanye anavyojisikia ili mradi havuki miiko ya ualimu. Tunaweza kusema tunajivunia kuwa naye ni mwalimu mzuri na kipenzi cha watoto,” anasema Malango.

Chanzo: mwananchi.co.tz