Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwalimu aliyedaiwa kuwalaza darasani wanafunzi aomba radhi

Madam Sabina Mwalimu aliyedaiwa kuwalaza darasani wanafunzi aomba radhi

Tue, 18 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera amemsamehe Mwalimu Sabina Haule aliyekuwa akidaiwa kuondoka na funguo za bweni na kuwafanya wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya wasichana Loleza Jijini Mbeya kulala darasani baada ya mwalimu huyo kumfuata Ofisini na kumuomba msamaha.

Akizungumzia kadhia hiyo, Mwalimu Sabina ambaye anatajwa kuwa mtenda amesema ametambua kosa lake hivyo kulazimika kwenda kumuomba msamaha Mkuu huyo na wanafunzi wake sambamba na kuahidi kushirikiana katika kuinua ubora wa taaluma shuleni hapo.

Mwalimu huyo aliondoka na funguo za bweni akidai kuwa chanzo ni ukorofi wa watoto hao lakini hakuwaamuru kwenda kulala darasani kwa kuwa baada ya kufunga bweni alirudi baadaye majira ya saa nne usiku na kuwaelekeza kwenda kulala mabweni mengine ambayo hayana wanafunzi lakini watoto hao walikaidi na kwenda kulala darasani kimyakimya hivyo kuomba msamaha kwa mkuu wa mkoa.

Mkuu wa Shule ya Loleza Mwalimu mkuu Betiseba Nsemwa alipoulizwa juu ya suala hilo amesema alikuwa akiendelea kushughulikia suala hilo kwa kuwakutanisha mwalimu wa nidhamu na msimamizi huyo wa bweni.

Baadaye mkuu wa mkoa Juma Zubery Homera akapata nafasi ya kutembelea hadi darasa ambalo wanafunzi wanadaiwa kulala usiku mzima kisha kuzungumza na wanafunzi hao akiwaasa kuzingatia nidhamu wawapo masomoni na kumuagiza afisa elimu mkoa Mwalimu Ernest Hinjo kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mwalimu husika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live