Mtoto wa mkazi wa Dar es Salaa, Aisha Sijavala wa, anayesoma Shule ya Msingi Olympio ya Dar es Salaam anadaiwa kupigwa hadi kupasuliwa jicho na mwalimu wake.
Taarifa za mtoto huyo kupasuliwa jicho, zimetolewa na ndugu wa familia ya Sijavala jina limehifadhiwa, ambaye alisema, tukio hilo limetokea mwanzoni mwa wiki hii.
“Olympio wanapiga sana watoto. Mwalimu kampiga mtoto wa Aisha Kijavala kampasua jicho juzi wamehangaika Mwananyamala Hospital jana Omar kafanya mpango wamemhamishia Muhimbili leo (juzi) ndio wamemuingiza chumba cha upasuaji)! Ndio wote wako hapo hospitali duh jamani,” kieleza chanzo hicho cha taarifa.
Baada ya kufuatilia taarifa za mtoto huyo shuleni hapo, mwalimu mmoja jina linahifadhiwa kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kuzungumzia jambo hilo alikiri tukio hilo kutokea lakini mwanafunzi huyo hakupasuliwa jicho.
“Hakupasuliwa jicho hizi ni taarifa za uongo wakati mwanafunzi anachapwa, kuna kijiti kiliruka na kumgusa upande wa jicho ni eneo dogo na mtoto aliwekewa dawa anaendelea na masomo,” alisema.
Kwa upande wake, Aisha Sijavala mama mzazi wa mtoto huyo akizungumza kwa simu alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Tulishamalizana na mwalimu, tukio limetokea kwa bahati mbaya. Nipo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) (ilikuwa jana (juzi) asubuhi) chumba cha upasuaji siruhusiwi kuongea na simu,” alisema.
Hata hivyo, Ofisa Elimu msingi wilaya ya Ilala, Sipora Tenga alikanusha taarifa za mtoto huyo kupasualiwa jicho.
Japo tukio hilo la mwanafunzi wa shule hiyo kudaiwa kupasuliwa jicho limekuwa na danadana, tukio hilo ni mwendelezo wa matukio yanayoendelea kuwakumba wanafunzi ambapo Januari 10 mwaka huu, ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja, Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Isaya Emmanuel aliyeonekana akiwachapa viboko kwenye nyayo wanafunzi wawili wa darasa la nne waliokuwa wakilia.
Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alitoa ufafanuzi wa tukio hilo la mwalimu mkuu huyo kuwaadhibu watoto hao wawili isivyostahili, huku akisema kuwa alishushwa cheo na kusimamishwa kazi.
Pia mwaka mwaka 2018 mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta mkoani Kagera alifariki baada ya kuchapwa viboko na mwalimu wake, kwa madai ya kuiba pochi yake.
Mwendelezo wa kukithiri kwa matukio ya wanafunzi kuadhibiwa vikali na walimu wao, unabainishwa katika utafiti wa Shirika la HakiElimu wa mwaka 2020.
Kulingana na utafiti huo, asilimia 87.9 ya watoto shuleni waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 90 kati ya hao, wakisema walifanyiwa ukatili kwa kupewa adhabu za viboko zinazotolewa shuleni.
Pia katika utafiti huo asilimia 54.9 ya watoto walisema walimu wao na walezi, wanatumia ngumi na makofi kama sehemu ya kuwarudi wanapowakuta wamefanya makosaa ya kinidhamu.