Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwaka mmoja wa kasi mradi wa umeme Rufiji

6d34f5455a2d99b79d2e925b4efc6046 Mwaka mmoja wa kasi mradi wa umeme Rufiji

Tue, 28 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JULAI 26, 2019, Rais Dk John Magufuli aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) katika eneo lililojulikana kama Stiegler’s Gorge, sasa likiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere wilayani Rufiji, Pwani.

Huu ni mradi mkubwa wa kufua umeme ambao unatarajia kutoa megawati za umeme 2,115 utakapokamilika Juni mwaka 2022, na unatekelezwa kwa asilimia 100 kwa fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo ni Sh trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake.

Mradi huu unaotekelezwa na wakandarasi, Kampuni za Arab Contractors na JV Elsewedy Electric zote za nchini Misri, na kufikia juzi Jumapili, ulikuwa umetimiza mwaka mmoja tangu uwekewe jiwe la msingi.

Harakati za mradi huo zilizoanzishwa miaka ya 1970 (zaidi ya miaka 40 sasa) na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere za kujenga mradi wa kufua umeme wa maji katika mto Rufiji, sasa si ndoto tena.

Juni 15, mwaka jana, mkandarasi alianza rasmi kazi hiyo ya ujenzi wa mradi. Desemba 12, 2018, mkataba wa ujenzi wa mradi ulisainiwa kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi, Arab Contractors na JV Elsewedy Electric. Tukio hili lilishuhudiwa na Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Misri.

Serikali ilikabidhi rasmi eneo la mradi kwa mkandarasi Februari 14, 2019. Ujenzi wa mradi huu utachukua kipindi cha miezi 42 ambayo miezi 36 ni ya ujenzi na miezi sita ni kwa ajili ya maandalizi. Mkataba wa ujenzi huo ulianza kutumika kuanzia Desemba 15, 2018.

Mwaka mmoja sasa baada ya Rais Magufuli kuweka jiwe la msingi la mradi huo, mambo yamepamba moto katika ujenzi huo kwani mkandarasi amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa ratiba ya kazi aliyoingia na Tanesco hivyo kufanya kazi kwenda kwa kasi na matarajio ya kukamilika kwa wakati.

Alipoweka jiwe hilo la msingi, Rais Magufuli alisema, “leo ni siku ya kwanza ya safari ya ukombozi wa kiuchumi kwa Tanzania.” Na kubainisha kuwa alikuwa ana furaha kubwa kwa sababu ameanza safari ya mwanzo ya ukombozi wa kiuchumi kwa Watanzania. Alisema pia ana sababu tatu za kuwa na furaha kubwa. Aliitaja ya kwanza kuwa ni kutekeleza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ya kuendeleza mradi huo wa kihistoria utakaofungua sekta nyingine.

“Ya pili ni kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa kati unaojengwa kwa viwanda, hivyo bila umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, hilo haliwezekani,” alisema Rais Magufuli.

Alisema zipo nchi ambazo gharama zao za umeme ziko chini hivyo Tanzania inalenga kufikia huko ili kujenga uchumi wa viwanda kufikia maendeleo.

Aliitaja sababu ya tatu kuwa ni kupitia mradi huo Tanzania imedhihirisha kuwa ni Taifa huru linalojiamulia mambo yake lenyewe.

Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Mushubila Kamuhabwa aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea mradi huo hivi karibuni kwamba hatua zote nane za utekelezaji wa ujenzi, zinaendelea kwa kasi inayohitajika.

Alitaja hatua hizo ni ujenzi wa njia kubwa ya ardhini ya mchepuko wa maji, sehemu ya kufua umeme, ukuta utakaotengeneza bwawa, eneo la kupokelea umeme unapozalishwa, barabara na madaraja, na kuchakata mawe yanayotumika kutengeneza zege na mahitaji mengine.

Kamuhabwa alisema mradi huo wa JNHPP una miradi mingi ndani yake na yote iko katika hatua mbali mbali, huku mafundi wakiwa kazini wakiendelea na ujenzi kwa kasi.

Akizungumzia kuanza kwa manufaa ya mradi, Kamuhabwa alisema, “Jambo la kufurahisha ni kwamba tayari mradi umeanza kuchangamsha uchumi wa nchi.”

Alitoa mfano kuwa wakati wakiweka zege kwenye njia ya kuchepusha maji, zaidi ya tani 200 za nondo zimetumika, hatua inayonufaisha viwanda nchini.

Manufaa mengine yaliyoanza kuonekana kwa wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka eneo la mradi ni upatikanaji wa miundombinu wezeshi kama vile umeme unaotoka Morogoro kupitia kwenye vijiji kadhaa.

“Lingine ni zaidi ya vijana wa Kitanzania wapatao 4,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, hususan yale yanayozunguka eneo la mradi, wameajiriwa na wanashiriki katika mradi kwa ari kubwa,” anasema Kamuhabwa.

Anasema wanatarajia idadi ya ajira itaongezeka kufikia watu 6,000 mradi utakapofikia hatua ya juu zaidi.

Baadhi ya wanakijiji cha Kisaki, kilichopo kilometa 60 kutoka kwenye mradi, walimpongeza Rais Magufuli kuanzishwa kwa mradi huo. Walikiri kuanza kuona manufaa yake ikiwa ni pamoja na ukuaji wa biashara.

“Kisaki inakuja juu, tuna uhakika mradi ukimalizika Kisaki itakuwa kama Morogoro. Kwa sasa biashara inakua kwa kasi sana tofauti na hapo awali. Kwa mfano, mchele tunauza kilo kwa shilingi 1,600 tofauti na hapo awali tulikuwa tunauza shilingi 500. Bei ya juu ilikuwa shilingi 1,000. Watu wameongezeka sana,” anasema Ali Matumbo.

Matumbo anakiri kijiji hicho kufikiwa na umeme ambao umenufaisha wananchi wengi ikiwamo shule.

Mwanakijiji mwingine, Asha Said anaeleza kufurahishwa na wageni wengi wanaofika katika kijiji hicho cha Kisaki na kuchangamsha biashara zao. Anasema ana matumaini, watapata barabara nzuri kutokana na mradi huo.

Hassan Ngozi anasema: “Kwetu sisi ongezeko la watu hapa Kisaki limekuwa na faida kubwa... Watu wakienda kufanya kazi huko kwenye mradi, wanakuja hapa kijijini wananunua bidhaa zetu na sisi tunapata pesa, haya ni manufaa makubwa kwetu.”

Akizungumzia wakati wa kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo Desemba 12, mwaka juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais John Magufuli alieleza kwa kina mradi huo na manufaa yake kwa Tanzania.

Kwa upande wa uchumi wa nchi alisema mradi utawezesha nchi kuwa na umeme mwingi na unaokidhi mahitaji na kuvutia uwekezaji wa miradi mikubwa na ya kati ya uzalishaji mali.

Aidha, kwa upande wa wananchi, mradi huu unategemewa kuchochea ukuaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kwa ujumla kama vile afya, elimu, maji, mawasiliano pamoja na sekta muhimu ya viwanda pamoja na shughuli nyingine za kijamii zinazotegemea umeme.

Kwa Tanesco ambao ndio wasimamizi wa mradi kwa niaba ya serikali, utasaidia kuimarisha sekta ya umeme na kuongeza mapato ya shirika kwa kuuza umeme mwingi zaidi ukilinganisha na awali, na pia kupunguza gharama za kufua umeme kwani umeme wa maji ni wa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati hiyo.

Rais Magufuli alisema serikali ilifanya uchambuzi wa kina kabla ya kuamua kuutekeleza na kubaini kuwa utakuwa suluhu kwa mahitaji ya sasa ya nishati.

Akasema waliangazia vyanzo vyote vya nishati vilivyopo nchini kama upepo, makaa ya mawe, madini ya urani, gesi asilia, na mafuta na kulinganisha na mahitaji ya sasa ya nishati hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.

“Baada ya kutafakari kwa kina hususan kwa kutumia vigezo vikubwa yaani uhakika wa chanzo chenyewe, gharama za utekelezaji (Investment costs), gharama za uzalishaji (generation costs) pamoja na tija tulibaini kuwa mradi huu ndio unaifaa zaidi nchi yetu kwa sasa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema mradi huo ni wa uhakika kwa kuwa una uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60 na utatumia maji yanayotoka katika mtandao wa mito iliyopo kwenye mikoa yenye wastani mkubwa wa mvua.

Kadhalika alisema gharama zake za utekelezaji (Sh trilioni 6.5) sio kubwa sana ukilinganisha na vyanzo vingine.

Kutokana na uwekezaji huo, alisema uzalishaji wa umeme nchini utaongezeka maradufu kutoka uzalishaji wa sasa wa megawati 1,560 na utakapokamilika bei ya umeme itapungua na kuwaletea wananchi nafuu ya upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa kuchochea shughuli uchumi ikiwemo viwanda, kilimo, umwagiliaji na michezo.

Mpango wa serikali ni kufikia uzalishaji wa umeme wa megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na hatimaye megawati 10,000 itakapofika mwaka 2025.

Rais Magufuli alitupilia mbali maoni ya wakosoaji wa mradi huo waliouhusisha na uharibifu wa mazingira akieleza kuwa “umeme wa maji ni rafiki wa mazingira” na kwamba eneo litakalotumika kutekeleza mradi huo ni dogo kati ya asilimia 1.8 hadi asilimia 2 la eneo lote lililokuwa likijiulikana kama Pori la Akiba la Selous.

Sambamba na hilo, alisema utapunguza ukataji wa miti inayotumika katika vyanzo vya kuni na mkaa zaidi na wakazi wa mjini katika matumizi ya nyumbani.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mbali na manufaa ya umeme, nchi pia itakuwa na maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwenye eneo lililo chini ya eneo la mradi wa maporomoko ya Mto Rufiji. Kadhalika litaboresha shughuli za utalii.

Chanzo: habarileo.co.tz