Dodoma. Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amezungumzia sakata la mtoto aliyekuwa akifungiwa kabatini, akisema kama kilichofanywa na mwalimu husika kitabainika kuwa ni kweli atamchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Kunambi ambaye ni mwajiri wa mwalimu huyo anayehusishwa na suala hilo, alisema hawezi kuingilia kwa wakati huu, badala yake anawaachia polisi waendelee na uchunguzi wao.
Mwalimu huyo mtumishi wa umma jijini hapa anayefundisha Shule ya Msingi Medeli, anadaiwa kumfanyia ukatili msichana wake wa kazi mwenye umri wa miaka 15 pamoja na mtoto wa binti huyo mwenye umri wa miezi mitano kwa kumfungia kabatini.
Hadi jana, binti huyo na mwanaye walikuwa wako katika wodi ya watoto wenye utapiamlo iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo madaktari wanaendelea kumpatia huduma mtoto huyo ingawa mama yake alisharuhusiwa baada ya kulazwa kwa siku mbili.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Dodoma, Samson Mkotya alisema wamepokea taarifa za mwalimu huyo, lakini wameviachia vyombo vya uchunguzi kuendelea na kazi yao.
“Sisi tupo kwa ajili ya kuwatetea wanachama wetu, hizi taarifa tumezipata na tutahakikisha mwanachama wetu anapata haki zake zote za msingi ikiwamo ya kupata dhamana, lengo ni asionewe wala asipendelewe bali haki itendeke,” alisema Mkotya.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi alisema mtoto na mama yake wanaendelea vizuri.
Alisema hadi jana mchana hospitali hiyo ilishapata vyakula vyote muhimu vya kumpa mtoto huyo mwenye utapiamlo na ameanza kuvitumia.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Makongoro anakoishi msichana huyo, Zena Chiuja alisema kwa sasa uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma umemzuia kumpelekea chakula.