Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Monduli Thomas Meiyan, ameiomba kamati ya ulinzi na usalama iliyopo chini ya mwenyekiti mkuu wa wilaya hiyo Frank Mwaisumbe kuharakisha uchunguzi wake uliokuwa unaendelea ili ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri hiyo uendelee.
Mkuu wa wilaya ya Monduli Frank Mwaisumbe hivi karibuni alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama na kugundua kasoro mbalimbali ikiwemo ujenzi kwenda kwa kusuasua na kumuagiza katibu tawala wilaya kumuandikia barua mkurugenzi wa Halmashauri kusimamisha malipo kwa mkandarasi huyo.
Akizungumza na kunukuliwa na Televisheni ya mtanadaoni ya "MONDULI TV ONLINE" Meiyan ameitaka taarifa hiyo ya kamati ya ujenzi ifike kwenye kamati ya fedha ili ijiridhishe na maazimio yaliyowekwa kwa ajili ya utekelezaji wa malipo hayo na sio kuzungumza kwa mdomo tu.
"Kimsingi tupongeze kazi ambayo imefanyika kwenye jengo hili na tunaendelea kuona kazi inayofanyika,nikupongeze sana Engeneer pamoja na mkurugenzi muendelee kukamilisha ili tuweze kufanya mikutano yetu ya halashauri hapa" alisema Meiyan
Kaimu mhandisi Halmashauri ya wilaya ya Monduli Mhandishi Lugano Mwakalinga ameiambia kamati ya fedha iliyofika kuona maendeleo ya ujenzi, kwamba changamoto iliyowakumba kwa sasa ni malipo ya fundi ambayo yalisimamishwa na mkuu wa wilaya na mpaka sasa kazi haiendelei kwa wiki tatu. "Kwa hiyo nilikuwa ninaomba kamati ya fedha mtusaidie tuweze kupata fedha ili fundi aweze kufanya kazi kwa ufanisi ule wa mwanzo".
Amesema mkuu wa wilaya alisimamisha kwa sababu malipo ya fundi waliandaa yamezidi kazi aliyoifanya huku Halmashauri wao wakidai kuwa wanalipa kwa kufuata mkataba.
"Kwa kazi aliyofikia fundi ndivyo tunavyomlipa, kwa hiyo tulifanya evaluation tukapita na kamati ya ujenzi wa jengo la utawala mbayo iliridhia fundi alipwe kwa kiwango alichoomba".
Kaimu mkurugenzi Halmashauri ya wilaya ya Monduli Victor Kaiza amesema wanatumia utaratibu wa "FORCE ACCOUNT" kumlipa mkandarasi kulingana na kazi aliyofanya ambapo naye hutegemea fedha hizo kuwalipa mafundi, hivyo kuchelewa kumlipa ni kusimamisha ujenzi. "Sisi kama kamati ya wataalamu tuliona kama unavyoenda ni sawa kwa sababu tulikuwa tunapitia ile evaluation iliyofanyika, tunaangalia mkataba na nini anatakiwa alipwe" alisisitiza
Mpaka sasa fedha zilizotumika mpaka sasa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la utawala la Halmashauri ya wilaya ya Monduli ni Shilingi Bilioni 1.5.