Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvutano Udart, Dart wachakaza mabasi

19481 Udart+pic TanzaniaWeb

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama mradi wa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam ni wa mabasi yaendayo haraka, basi mabasi 140 yanayotoa huduma hiyo yanachakaa kwa kasi.

Kasi ya kuchakaa kwa mabasi hayo inatokana na mvutano uliodumu kwa miezi saba baina ya Mradi wa Mabasi ya Yaendayo Haraka (Dart) na kampuni inayotoa huduma hiyo ya usafiri ya Udart uliosababisha mabasi 70 mapya kukwama katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mabasi yanayotoa huduma kwa sasa yanalazimika kufanya kazi kupita kiasi, huku yakichukua abiria wengi zaidi, Udart imeeleza.

Mabasi hayo yaliyowasili Februari 16, yaliagizwa na Udart kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma hiyo, lakini imeshindwa kuyatoa bandarini kutokana na Dart kueleza kuwa taratibu hazijafuatwa.

“Mabasi yanaharibika mara kwa mara kwa kuwa yanabeba abiria wengi kupita uwezo wake,” msemaji wa Udart, Deus Bugaywa aliiambia Mwananchi jana.

Bugaywa alisema wakati wanaanza mradi huo walikuwa wakihudumia abiria 50,000 kwa siku, lakini kwa sasa wanahudumia abiria 180,000 mpaka 200,000.

“Tena kwa idadi ileile ya mabasi, jambo ambalo pia ni hatari kwa usalama na afya za abiria,” alisema.

Alisema athari nyingine ni kuwapo kwa msongamano ambao unaondoa maana nzima ya mradi huo wa mabasi wa kisasa.

“Watu hawaoni tofauti ya usafiri daladala na mwendo wa haraka,” alisema.

“Wakati tunakabidhiwa kuundesha mradi huu, lengo letu ilikuwa watu waache magari yao nyumbani wapande mabasi yetu, lakini kwa msongamano huu hakuna aliye tayari kufanya hivyo. Tulidhani kama mabasi yetu 70 yangeruhusiwa yangepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.”

Alisema abiria wanalazimika kusimama vituoni kwa muda mrefu kusubiri usafiri kwa kuwa mara nyingi mabasi hupita yakiwa yameshajaa abiria.

Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, Charles Newe alisema kuanza kwake kazi yatasaidia kuongeza nguvu katika mabasi 140 yaliyopo kwa sasa.

Katika mvutano wa kuhusu kukwama kwa mabasi hayo, kila taasisi—Udart na Dart—ilikuwa na kauli yake na kutupiana lawama.

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa Dart, Ronald Lwakatare alisema kama ilivyo kwa Udart, nia yao ni kuondoa msongamano, lakini hawawezi kuruhusu mabasi hayo kuingia barabarani mpaka utaratibu ufuatwe, lakini alipoulizwa ni utaratibu gani, hakuusema akiurushia mpira Udart.

Lakini Bugaywa alisema anachojua wamekamilisha taratibu zote na wanachosubiri ni ruhusa ya Dart ambao ndio wasimamizi wa mradi huo wakiiwakilisha Serikali.

“Sisi tunavyojua kila kitu tumeshakamilisha, tunasubiri tu Dart watuambie ingizeni mabasi barabarani kama ilivyoturuhusu kuanzisha njia ya Muhimbili- Kariakoo, kwani bila kibali chao hatuwezi,” alisema.

Aliongeza kuwa mabasi hayo yana uwezo wa kubeba abiria 155, kwa hiyo yakiingizwa barabarani yataongeza uwezo wa kubeba abiria maradufu ya uwezo wa sasa na hivyo kuondoa tatizo la msongamano.

Awali, wakati mradi huo unaanza, Udart ilipaswa kuwa na mabasi 305, lakini Serikali imekuwa ikiruhusu uingizaji wa mabasi hayo kidogokidogo, ikihamasisha kampuni nyingine kuingia ili kuongeza ushindani ambao utaboresha huduma hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz