Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zilivyoharibu barabara Mwanza, wakazi walalama

Mvua Mwanzaaa.png Mvua zilivyoharibu barabara Mwanza, wakazi walalama

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Mwanza zimekata mawasiliano ya barabara inayounganisha Mtaa wa Mahina Kati na Kagomu jijini humo.

Kutokana na kukatika kwa barabara hiyo, wananchi wamejitengenezea njia mbadala inayochepuka kwa kupanga mawe kwenye maeneo yaliyoharibika.

Akizungumza hivi karibuni , Mkazi wa Mahina Kati jijini humo, Fatma Hassan amesema barabara hiyo imeharibika kufuatia mvua zilizonyesha kwa zaidi ya saa mbili Jumatatu Januari 29, 2024,.

Mbali na kukatika, Fatma amesema barabara hiyo imekuwa likichimbika kila mvua inaponyesha na kuwa abiria wamekuwa wakipata maumivu ya mwili kutokana na mashimo yaliyopo kwenye barabara hiyo.

“Barabara hii mpaka tumeichoka, Serikali ituonee huruma, ni mbovu unaweza kutoka huku Mahina ukatumia zaidi ya saa moja huku mwili wote ukiwa unauma kutokana na kubamizwa kwenye mashimo,” amesema Fatma.

Dereva wa daladala kati ya Mahina-Mjini, Justin Baltazar amesema baadhi ya daladala zinazotoa huduma ya usafirishaji kupitia barabara hiyo zimesitisha kutoa huduma kutokana na ubovu huo.

“Wenzetu wamesitisha kuja huku Mahina kwa sababu magari yakija huku yanavunja ‘shokapu’ kwa sababu barabara ina mashimo. Springi unanunua Sh55,000 ukija tripu moja Mahina Kati hata ungetembea mwendo wa taratibu lazima ikatike ukanunue nyingine,” amesema Baltazar.

“Tumeshajaribu kuweka mgomo baridi wa daladala ili barabara hii ijengwe lakini haikuwa hivyo, matokeo yake tunaoendelea kutoa huduma ya usafirishaji tumeanza kufikiria kuacha kuleta magari yetu huku,” ameongeza.

Kilio cha barabara hiyo kinaongezewa sauti na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahina Kati, Moi Mgewa, ambaye amesema pamoja na kutoa taarifa kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) jiji la Mwanza, hakuna hatua zilizochukuliwa.

Amesema kukatika kwa barabara hiyo kumeulazimu uongozi wa kata hiyo kuweka walinzi shirikishi watakaosaidia kuelekeza magari yasipite eneo hilo usiku, ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na kuchimbika kwa barabara hiyo.

“Awali, palikuwa panapitika lakini sasa hivi kutokana na mvua zinazonyesha barabara yote imebomoka, hata juzi kuna gari ya Wachina ilisombwa na maji, wananchi ndiyo waliwahi kuwanusuru.

“Kuna wananchi wamejitolea kuweka mawe eneo la pembeni ili kuwezesha magari kupita,” amesema Mgewa.

Meneja wa Tarura jijini Mwanza, Danstan Kishaka amesema tathmini imeshafanyika kwa barabara zinazosimamiwa kinachosubiriwa ni fedha za kuanza ujenzi.

“Kuna juhudi kubwa Serikali inafanya kuhakikisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua inarejeshwa katika hali ya kawaida na hiyo barabara ya Igelegele kwenda Mahina Kati ni miongoni mwake. Nitafika kuangalia endapo uharibifu uliokuwa umetokea hadi wakati wa tathmini umeongezeka,” amesema Kishaka.

“Barabara hiyo (Igelegele-Mahina Kati) iko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami lakini mpango huo haujakamilika, utakapokamilika tutawapa taarifa kwa maandishi na tutakuwa tukiliongelea suala hilo kwa njia rasmi, lakini kwa sasa libaki hivyo kwamba liko kwenye mpango,” alisema

“Kwa sasa hatujapata fedha za dharura tulizoomba, kwa hiyo kipindi hiki tunaweza tukapata taabu kidogo tuvumiliane, Serikali inaenda kwa bajeti kwa hiyo pale ambapo tutaambiwa tumepata fedha za dharura tutaingia barabarani haraka sana,” amesema.

Daraja la Mkuyuni

Adha, uharibifu wa mvua si kwa wakazi wa Mahina pekee, bali hata wakazi wa wanaotumia Barabara ya Kenyatta inayotoka katikati ya Jiji la Mwanza kwenda Shinyanga, kwa kuwa wakati mwingine hulazimika kutumia zaidi ya saa tatu kusubiri maji yanayopita juu daraja la Mkuyuni kupungua.

Maji hayo siytu huharibu miundombinu ya eneo hilo, pia husomba bidhaa za wakazi na wafanyabiashara wa eneo la Mkuyuni Kata ya Mkuyuni jijini humo.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu amekiri kuwa na taarifa ya changamoto ya daraja hilo na kubainisha kuwa liko kwenye mpango wa kuongezwa kina na kupanuliwa.

“Wakala (Tanroads) ulishafanya design (usanifu) upya kujenga njia nne za barabara ili kupunguza adha ya kusafiri muda mrefu kwenda Nyegezi na maeneo mengine kutokana na daraja la Mkuyuni kufurika. Tuta litainuliwa na daraja litainuliwa kidogo ili kuruhusu maji yapite,” amesema Ambrose.

“Serikali imeshaliona, tunatarajia mwaka ujao wa fedha 2024/25, fedha zitatengwa, ila kwa sasa hivi siwezi kusema ni lini tutaanza. Tunachokifanya sasa hivi ni kusafisha mitaro ili maji yapite bila kutuama,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live