Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zawavuruga wananchi, wengine wajihifadhi juu ya miti

81961 Pic+mvua Mvua zawavuruga wananchi, wengine wajihifadhi juu ya miti

Mon, 28 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini ikiwamo mkoa wa Tanga zimesababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na kero kwa wananchi huku baadhi ya wananchi wakilazimika kujihifadhi juu ya miti.

Mvua hizo zimesababisha kukatika barabara kadhaa, madaraja na hata baadhi ya nyumba za wananchi kuzingirwa na maji.

Mpaka jana idadi ya watu wanaotajwa kufa kutokana na mvua hizo walifikia 14, baada ya kuripotiwa vifo vingine vitatu.

Polisi walithibitisha kupatikana mwili mmoja katika kitongoji cha Bwawani kata ya Sindeni, na miili ya watoto wawili iliyokutwa mtaa wa Wandama kata ya Kwenjugo wilayani Handeni.

Juzi wananchi 10 waliripotiwa kufariki dunia wilayani Handeni mkoani Tanga baada ya gari aina ya Noah walilokuwa wakisafiria kutumbukia mtoni katika eneo la Sindeni, barabara kuu ya Handeni -Korogwe. Mashuhuda wa ajali hiyo wanasema kuwa ingawa walitoa tahadhari kwa dereva huyo kutopita katika eneo hilo lakini aligoma.

“Barabara katika eneo hilo ilikuwa imefungwa na hata tulipomwambia dereva asiende alikataa na kusema ngoja akajaribu,” anasema shuhuda mmoja.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Hata hivyo, muda mfupi baadaye anasema walisikia gari hilo limezama na abiria wote waliokuwa ndani ya gari wamepoteza maisha.

Baadaye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema watu 10 wamefariki baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye maji kutokana na barabara kukatika, mwingine kusombwa na maji.

Kuhusu ujenzi wa miundombonu, Gondwe anasema Serikali inasubiri maji yapungue, ili Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Tanga na Handeni waanze kurekebisha eneo hilo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Mwangoka anasema wamekutwa na mvua zisizo za kiasi, hivyo kuendelea kumuomba Mungu awanusuru.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua ya kuzuia maafa zaidi hasa kutokea kwa watu. Ndio maana magari yamezuiliwa kutopita katika maeneo hatarishi. Lipo eneo la Daraja la Mandera, zuio njia ya Korogwe–Handeni daraja la Sindeni limekatika na njia ya Korogwe-Muheza kupitia Mnyuzi Mto Luhengera umejaa,” ameandika mkuu huo wa wilaya katika ukurasa wake wa Instagram.

“Haya ni maafa yanaletwa na Mungu hakuna anayeweza kuzuia kikubwa tuwe watulivu na wavumilivu huku tukichukua tahadhari. Zaidi ya yote wananchi maeneo tulioambiwa tuhame kama tahadhari nawasihi mfanye hivyo ni jitihada ya kuokoa maisha ya watu waliopo maeneo hatarishi.”

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella anasema ameshaagiza Tanroads kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kufanya tathmini ya ujenzi wa daraja la Mandera wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Kuvunjika kwa daraja hilo kulisababisha magari zaidi ya 300 yaliyokuwa yakitoka mikoa ya Kaskazini na nje ya nchi kuelekea Dar es Salaam kukwama.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Tanga, Solomoni Mwangamile, anasema baada ya kuona hali ni mbaya waliifunga barabara hiyo na magari yote kutakiwa kupitia Handeni Mjini kuelekea mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

“Madereva wanatakiwa kuwa wasikivu na maelekezo yote wanayopewa na askari, yaani mtu asitake kwenda kujaribu eneo la tukio ili kuhakikisha hali za usalama inatamalaki.

Pia aliwataka madereva kuendesha magari yao kwa mwendo mdogo kwa kuwa kutokana na mvua, barabara zinateleza na hata uoni wao unakuwa si mzuri.

Wananchi

Wakazi wa eneo daraja lilipokatika wanasema majira ya saa 7.30 usiku walisikia kishindo kikubwa na saa 11 alfajiri walipokwenda walishuhudia daraja hilo likiwa limekatika.

Wanasema hali si nzuri kwa kuwa mawasiliano kati ya wilaya hizo yamekatika.

“Tunategemea daraja kupitisha mazao mbalimbali kama maharage na ndizi. Hali hii ni ngumu kwetu,” anasema mmoja wa wanachi hao.

Mwingine anasema hali kama hiyo hawajaiona miaka mingi, hivyo kuiomba Serikali baada ya maji kupungua kukarabati daraja.

Abiria waliokwama

Baadhi ya abiria walikwama katika eneo la Segera kwa siku mbili, baada ya barabara eneo la Mandera kukatika.

Mwajuma Ismail, anasema alikuwa anakwenda jijini Dar es Salaam kuhudhuria mazishi ya mdogo wake lakini ameshindwa.

“Nitakuta wameshazika, nimeumia sana kushindwa kumzika ndugu yangu,” anasema.

Doreen Mlekwa, anasema alikuwa akienda Dar es Salaam kuchukua mzigo kwa ajili ya biashara yake ya duka, hivyo kupata changamoto hiyo kumemrudisha nyuma.

“Nilikuwa niende na kugeuza siku inayofuata…si unajua maisha yenyewe ya sasa ni kukimbizana! Sasa nimekwana sina jinsi,” anasema.

Beatice Onesmo, anasema wiki tatu zilizopita watu waliokuwa wakitokea Moshi, Arusha walikuwa wakipitia Korogwe Stendi na kisha kutokea Mkata na kuendelea na safari, lakini sasa barabara imekatika eneo la Misima, Handeni, hivyo hata kuzunguka haiwezekani.

Pia anasema abiria wanaotoka mikoa ya Kaskazini; Manyara, Kilimanjaro na Arusha wamekwama na hata wale waliokuwa wakitoka Dar es Salaam kuelekea mikoa hiyo hawakuweza kuendelea na safari.

Wahama makazi

Baadhi ya kaya zililazimika kuhama makazi yao kwa muda katika Wilaya ya Korogwe kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji.

Wananchi hao wanasema mbali na nyumba zao kuzingira ya maji, pia mali zote zilizokuwamo zimeharibika.

Zainabu Said, anasema maji yalianza kuingia katika nyumba yake asubuhi na kuharibu vitu vingi. “Inanibidi nihame kuokoa vitu vyangu, siwezi kukaa tena hapa,” anasema.

Naye Juma Hamis anasema mvua imewapa hasara kubwa kutokana na mali zao nyingi kuharibika.

“Tunaomba msaada wa Serikali kwani tumepata hasara kubwa,” anasema.

Kwa upande wake, Pili Athumani anasema vitu vingi vimeharibika, hata sasa hana akiba ya chakula.

Pia anawaza madaftari ya wanaye watatu yaliyoharibika kwa maji. “Sijui itakuwaje kwa wanangu, madaftari yao yote yameharibika. Wanaanza upya na mmoja mwakani anaingia darasa la saba,” anasema.

Mkazi mwingine, Juma Kibwana analalamika miundombinu kuharibika hali itakayomkwamisha katika mambo yake mengi. “Kwa sasa hatuna mawasiliano na wilaya nyingine. Shughuli zetu nyingi za kiuchumi zitakwama,” anasema.

Naye Ofisa Habari wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto wilayani Handeni Joan Luvena, alisema juzi watu 51 walijihifadhi juu ya miti katika mtaa wa Kwamaraha kutokana na makazi yao kuzingirwa na maji.

Anasema wananchi baada ya nyumba zao kujaa maji, walikwenda kwa ofisa mtendaji wao kuomba msaada ambaye naye alipiga simu Kikosi cha Uokoaji.

“Tulipigiwa simu usiku kama saa 3 hivi, tulipokwenda tulikuta maji yamejaa sana eneo hilo. Tuliwashauri wananchi wapande kwenye miti na wajifunge na mashuka ili wasidondoke,” anasema.

Anasema maji katika eneo hilo yanatoka pia sehemu nyingine kwa kuwa ni bondeni na kwamba maji hayo yalikuwa na magogo makubwa na miti mikubwa iliyoanguka.

“Tuliwaambia wakati ule hatuwezi kuwaokoa, wawashe tochi ili tubaini maeneo waliyokuwapo. Saa 10.30 alfajiri tulirudi kuwaokoa.

“Zilikuwa kaya saba zenye watu 51, sasa familia hizo zimehifadhiwa kijijini,” anasema.

Kauli ya Waziri

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi, Elias Kwandikwa anasema Serikali imejipanga kuhakikisha barabara ya Handeni-Kilindi na ya Handeni-Korogwe inapitika ndani ya muda mfupi.

Anasema washafanya makadirio ya awali kuhakikisha njia hizo zinapitika kwa sababu ni kiungo muhimu kwa mikoa ya Kaskazini.

Chanzo: mwananchi.co.tz