Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zavunja daraja Chato, zakata mawasiliano ya vijiji

Mvua zavunja daraja Chato, zakata mawasiliano ya vijiji

Wed, 22 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali mkoani Geita zimesababisha daraja la Samazina lililopo wilayani Chato kuvunjika na kukata mawasiliano kati ya kijiji cha Lwantabe na Buziku.

Kukatika kwa daraja hilo lililoko barabara ya Buziku –Nyarutesya kunawalazimu wananchi wanaotaka kuvuka eneo hilo kulipa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 kwa vijana waliogeuza tatizo hilo kuwa fursa ya kujipatia chochote.

Akizungumza na Mwananchi jana, diwani wa Buziku, Joseph Magomamoto alisema kata hiyo yenye wakazi zaidi ya watu 15,000 ina vijiji sita wanaotegemea daraja hilo.

Alisema awali hakukua na barabara na kwamba aliitaarifu halmashauri tatizo hilo na mwaka 2019 ikajengwa na Wakala wa Barabara lakini daraja hilo halikujengwa na kuendelea kuwa changamoto kwa wananchi.

“Huu mto ukifurika wananchi hawawezi kwenda shamba, lakini pia hata wagonjwa, hasa wajawazito, inawalazimu wajifungulie nyumbani, watoto hawaendi shule,” alisema Magomamoto.

Diwani wa kata hiyo, Magomamoto alidai amekuwa akifikisha malalamiko hayo kwa Wakala wa Barabara za Mijini Na Vijijini (Tarura) ambao walimjibu kuwa tayari wametenga fedha lakini anashangaa kuona ujenzi ukichelewa licha ya madaraja kujengwa sehemu nyingine.

Pia Soma

Advertisement
Asteria Kawa, mkazi wa kijiji cha Lwantabe, alisema wananchi wanakabiliana na changamoto hiyo kwa zaidi ya miaka miwili sasa na wanalazimika kuvuka kwa miguu na wakati maji yakiwa mengi hushindwa kuvuka na hivyo kusababisha wanafunzi wakose masomo huku huduma za afya nazo zikiwa ni tatizo.

Naye Charles Ng’ombeyapi, mkazi wa Bugege, alisema mto huo ni kero zaidi kwa wanafunzi ambao sasa licha ya shule kufunguliwa, wengi bado wapo nyumbani wakihofia kusombwa na maji wakati wakivuka mto huo.

Mratibu wa wakala wa barabara mkoani, Geita Gaston Pascal alisema tayari amemuelekeza meneja wa Tarura wa Chato kuchukua hatua za haraka za kuweka daraja la muda wakati akisubiri fedha za kujenga daraja la kudumu.

Chanzo: mwananchi.co.tz