Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zapandisha gharama za usafiri Mng’eta, Mlimba

Mvua Mgetaaa.png Mvua zapandisha gharama za usafiri Mng’eta, Mlimba

Mon, 8 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kukata mawasiliano ya baadhi ya barabara nchini, wananchi wa Mng’eta na Mlimba mkoani Morogoro ambako nako miundombinu ya barabara imeharibiwa vibaya na mafuriko hayo, wameanza kupata maumivu ya kupanda kwa bei za usafiri.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 8, 2024, mkazi wa Kibiti mkoani Pwani, Everline Kikwesha amesema ameenda Mlimba kumtembelea mtoto wake shuleni na kujikuta akilazimika kutumia nauli ya Sh75,000 badala ya Sh15,000 ya awali.

“Kutoka Ifakara hadi Mlimba nimetozwa nauli ya Sh75,000, ningekuwa sina hela ya ziada sijui ingekuwaje. Nauli ninayoifahamu siku zote ni ya Sh15,000,” amesema Kikweshi.

Licha ya kutozwa nauli hiyo, amesema magari hayo yanaishia Mng’eta kwa sababu mawasiliano ya barabara kuelekea Mlimba yamekatika.

“Magari kutoka Ifakara kwenda Mlimba yanaishia Mng’eta na ili ufike Mlimba lazima uchukue bodaboda (Pikipiki) na nauli yake ni kati ya Sh30,000 au Sh40,000 kwa sababu kipande cha Mng’eta kufika Mlimba katikati hapo maji yamesomba daraja na magari hayawezi kuvuka kwende ng’ambo nyingine,” anasema Kikwesha.

Amesema eneo hilo ambalo limekatika mawasiliano kuna mto, hivyo bodaboda nazo zinavushwa na watu kwa kuzibeba kwa gharama ya Sh2,000.

Mwananchi pia limezungumza na dereva wa Noah inayosafirisha abiria kati ya Ifakara na Mlimba, Timotheo Ndopwe ambaye amesema baadhi ya matajiri wenye magari wamesitisha safari ya kwenda Mlimba kutokana na ubovu wa barabara.

“Nimeona kampuni ya ujenzi wa barabara Mng’eta wakishusha mitambo yao ya kutengenezea barabara, nawaomba Tanroads Morogoro wawasimamie makandarasi hao watengeneze maeneo yote korofi kwa ubora zaidi, ili hali ya kukatika kwa mawasiliano isijirudie tena maana mvua bado zinaendelea kunyesha,” amesema Timotheo.

Dereva huyo anasema ardhi ya wilaya ya Kilombero imetawaliwa na milima ya Udzungwa na uwanda mpana wa tambalale uliojaa mito mikubwa na midogo ambayo inachangia barabara nyingi kuwa na mashimo makubwa.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lazeck Kyamba amesema timu ya wataalamu imehamia katika maeneo yote korofi na wameanza kufanya ukarabati.

Amesema kwa barabara ya Ifakara hadi Mlimba ambayo imekatika, Kyamba amesema tayari timu ya wahandisi iko wilayani humo kwa lengo la kufanya marekebisho kwenye maeneo yote korofi na kurejesha mawasiliano kwa barabara zilizokatika.

“Kampuni tatu za kutengeneza barabara zipo wilayani Kilombero kwa lengo la kurekebisha maeneo yote korofi na tumekubaliana wafanye kazi usiku na mchana na wahakikishe barabara ya Ifaraka, Mng’eta hadi Mlimba inafunguka,” amesema Mhandisi Kyamba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live