Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zamsomba dereva wa bodaboda, abiria wake

MVUA MAFURIKOOOO .jpeg Mvua zamsomba dereva wa bodaboda, abiria wake

Wed, 13 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanamke ambae jina lake halijafahamika amepoteza maisha baada ya kusombwa na maji wakati akivuka daraja linalounganisha Kata ya Karumwa na Kafita Wilayani Nyang’hwale, mkoani Geita akitumia usafiri wa bodaboda.

Mbali na mwanamke huyo dereva wa bodaboda hiyo bado hajapatikana na Jeshi la Zimamoto na Uokozi linaendelea kumtafuta.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame amethibitisha kutokea kwa kifo cha mwanamke huyo Desemba 11, 2023 na kusema mwili wake umepatikana ukielea juu ya maji.

New Content Item (2)

“Mwanamke aliyekuwa amebebwa kwenye pikipiki tumempata akiwa ameshapoteza maisha na sasa tunamtafuta dereva wa pikipiki, tunasikia alichukuliwa na maji na kutupwa huko mbele, tumuombee awe salama.

“Niwaombe tuchukue tahadhari kipindi hiki cha mvua miundombinu ya barabara imelemewa, tusidharau maji,” amesema Kingalame.

DC huyo amewataka wananchi kuacha tabia ya kupima kimo cha maji kwa mguu na badala yake wanapokuta barabara au mto umefurika, ni vema kutafuta njia nyingine au kuahirisha safari kwa usalama wao.

Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo zimesababisha barabara nyingi kuharibika na nyingine kujaa maji ikiwemo ya Geita - Nyanghwale na kusababisha wananchi kuzunguka hadi Kakola.

Nastory Sagaika mkazi wa Geita ameitaka jamii kuchukua tahadhari kipindi hiki cha mvua hasa kwa watoto kwa kuwazuia kupita kwenye maeneo ya mikondo ya maji ili kuepuka maafa yanayoweza kutokea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live