Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zaleta kizaazaa Mbagala

32346 Mvuapic Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha mikoa mbalimbali nchini Tanzania leo asubuhi Jumatano Desemba 19, 2018 zimesababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara eneo la Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam kutokana na kujaa maji.

Hali hiyo imewalazimu watembea kwa miguu kuvua viatu na kukanyaga maji hayo yaliyofunika barabara.

Wakati wakiendelea kuvuka kwa tabu, magari nayo yanatembea mwendo mdogo na kusababisha foleni huku daladala nazo zikikosa hata eneo la kuegesha kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria.

Mwananchi leo limeshuhudia askari wa usalama barabarani wakiwa miongoni wa wanaoyashangaa maji hayo huku baadhi wakionekana kujadiliana nini cha kufanya.

Ernest Mabiyo, mkazi wa Mbagala amesema hali hiyo imekuwa ikitokea mara kwa mara mvua zinaponyesha.

“Haya mambo yameshakuwa sugu, mitaro imejaa takataka inashindwa kupitisha maji matokeo yake yanakimbilia barabarani na kusababisha adha hii,” amesema.

Mwananchi iliwahi kufanya mahojiano na Mhandisi Mwandamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Eliamini Tenga ambaye alilitaja eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo sugu ambayo athari za mvua husababishwa na binadamu.

“Pale Mbagala watu wanafanya biashara hadi pembezoni mwa barabara na uchafu wote wanatupia kwenye mitaro, wengine wanahifadhi meza na matenga yao humo sasa mvua zinaponyesha maji hayapiti na yanakwenda katika barabara,” alisema.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz