Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yawakosesha usingizi wakazi Dar

49575 Mvuapic

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kutangaza uwepo wa mvua kubwa ndani ya siku tano katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam wakazi wa mtaa wa Juhudi kata ya Kiburugwa wilayani Temeke wameeleza hofu yao kufuatia mvua hizo.

Wakazi hao ambao makazi yao yamekuwa njia ya maji taka wamesema katika kipindi hiki cha mvua wako hatarini kupata maradhi ikiwemo kipindupindu.

Kufuatia hilo wameiomba halmashauri ya wilaya ya Temeke kuangalia namna ya kuwasaidia ikiwemo kuweka mifereji ili kuzuia maji yasisambae kwenye maeneo yao.

Malalamiko yamekuja kufuatia eneo hilo kukosa mifereji ya kupitishia maji na matokeo yake mvua zinaponyesha maji yanaelekea kwenye makazi ya watu.

Akizungumza na Mwananchi mkazi wa eneo hilo Hawa Kombo amesema mvua zinaponyesha wakazi wa mtaa huo wanakuwa hatarini kutokana na maji mengi kuelekezwa kwenye nyumba zao.

“Tupo roho juu, yani tukiona manyunyu tunakosa raha, mvua ikinyesha maji yote ya juu yanakuja kwenye nyumba zetu. Huko njiani ndio usiseme tunalazimika kukanyaga maji.

Related Content

“Sasa wapo ambao wanatumia mwanya huo kufungulia vyoo vyao basi hapo ndio hatari inapozidi kuwa kubwa magonjwa kama kipindupindu yanakuwa sehemu ya maisha yetu mvua zikianza,”

Kwa upande wake Rashid Mgaza ameeleza kuwa hali ya kufurika maji wakati mwingine inasababisha watoto kushindwa kwenda shuleni.

“Mvua zikinyesha wakazi wa Juhudi hatuna amani kwanza hata mtoto akienda shule unakuwa roho juu hayo maji yanayotiririka hata mtu mzima ni hatari kupita sasa ndio apite mtoto,

“Tunaomba serikali itusikie huku nako wanaishi watu na kwa kuwa serikali yetu ni ya wanyonge basi itusikie na kutupatia ufumbuzi wa changamoto hii,” amesema Mgaza

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Juhudi,  Athuman Namna amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa imesababishwa na maji yanayotoka maeneo ya juu kukosa mwelekeo na matokeo yake yanashuka chini kwenye makazi ya watu.

Amesema amechukua hatua mbalimbali kuwasilina na viongozi wa manispaa ya Temeke lakini bado hawajapata ufumbuzi wa tatizo hilo.

“Tukisikia mvua amani inatoweka huku kwetu na kama hii iliyotangazwa watu wanalazimika kuacha nyumba zao lakini ikitengenezwa mifereji hili tatizo litakuwa historia,” amesema Namna



Chanzo: mwananchi.co.tz