Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yaua watoto wawili wakiwa wamelala, barabara zafungwa Serengeti

90010 Mvua+pic Mvua yaua watoto wawili wakiwa wamelala, barabara zafungwa Serengeti

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Mvua kubwa iliyonyesha mkoani Mara nchini Tanzania imesababisha maafa ikiwamo vifo vya watu watatu wakiwamo watoto wawili wa familia moja na uharibifu wa miundombinu.

Pamoja na watoto hao, mwili wa dereva bodaboda aliyesombwa na maji wakati akivuka katika eneo la Issenye wilayani Serengeti mkoani Mara umepatika.

Diwani wa Issenye Ally Nyarobi amesema mvua iliyonyesha imesababisha daraja la Nyiberekera kukatika na dreva bodaboda alilazimisha kupita leo asubuhi Alhamisi ya Desemba 26, 2019 na kusombwa na maji yaliyosababisha kifo chake.

Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema mwili wa dereva huo umepatikana hatua chache toka eneo alilozama na jina lake halijafahamika.

Amesema kwa mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Alhamisi imesababisha maafa hayo na baadhi ya madaraja kubomoka.

Babu amesema mvua hiyo imesababisha pia vifo vya watoto wawili wa familia moja na mmoja kujeruhiwa baada ya nyumba walimokuwa wamelala kujaa maji kisha kubomoka eneo la Issenye wilayani humo.

Amesema miili ya watoto hao imepelekwa kituo cha afya Nyamuswa wilaya ya Bunda mkoani humo wakati taratibu za mazishi zikiendelea.

Diwani wa Issenye (CCM), Ally Nyarobi amesema watoto hao ni wa Hagai Kongoye wenye umri wa miaka 10 na mwingine minne.

Mvua hizo zimesababisha barabara za kutoka Mugumu kwenda Arusha kupitia Fort Ikoma na Makunduzi kutopitika baada ya kukatika daraja na nyingine maji kujaa hadi juu.

"Barabara ya Natta Makundusi nayo haipitiki maana maji yamefunika daraja, magari ya kwenda Arusha au kutoka ikiwamo mabasi hayawezi kupita mpaka maji yapungue," amesema Babu

Amesema amewasiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) kuhusu suala hilo na wamemwahidi kufika haraka wilayani hapo ili kushughulikia daraja la Fort Ikoma liweze kupitika.

Kaimu Meneja wa Tanroad, Reginald Massawe amesema wamelazimika kutuma wataalam wao barabara zote za wilaya ya Serengeti ili kusaidia kurekebisha magari yaweze kuvuka kwenda na kutoka Arusha.

Chanzo: mwananchi.co.tz