Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yaua, polisi yatahadharisha

Maji Ya Mvua.jpeg Mvua yaua, polisi yatahadharisha

Tue, 3 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu watatu wamefariki kwa kusombwa na maji ya mvua mkoani Arusha, kutokana na mvua zilizoanza kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Watu hao, wamefariki katika Wilaya za Monduli na Longido, ambapo wawili ni wanafunzi akiwemo aliyetarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza siku chache zijazo baada ya kufaulu darasa la saba.

Akizungumzia vifo hivyo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha, Justine Masejo alisema matukio hayo yalitokea juzi na kukatisha maisha ya Baraka Elias (17) aliyekuwa mkazi wa Lesiimingoli Wilaya ya Monduli ambaye alikuwa amechaguliwa kuanza kidato ya kwanza mwaka huu.

Alimtaja mwingine aliyefariki ni Lemali Sayeleki (5) ambaye alikuwa anasoma shule ya msingi Ranchi mkazi wa Kijiji cha Olbomba Wilaya ya Longido.

Kamanda Masejo alimtaja mwingine aliyefariki ni Sanada Lekishoni(75) mkazi wa Kijiji cha Lesiimingori Wilaya ya Monduli.

“Natoa wito kwa wananchi kuchukuwa tahadhari kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha kutovuka maeneo yenye mito lakini pia kuepuka kutembea kwenye mvua” alisema

Siku za karibuni kumekuwa na mvua kubwa zikinyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa Arusha zikiwemo Wilaya za Monduli na Longido ambazo zimekumbwa na ukame mkubwa uliosababisha vifo vya mifugo, familia kukosa vyakula na maji.

Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa zaidi ya mifugo 58,000 ilikufa kutokana na ukame ulioyakumba maeneo tofauti.

Katika wilaya hizo pia kumekuwa na changamoto ya upungufu wa chakula kutokana na mavuno kushuka kwa miaka mitatu mfululizo yaliyochangiwa na kukosekana mvua za kutosha.

Ofisa Mifugo na Mabadiliko ya tabia nchi wilaya ya Longido, Nestory Dagarro aliwataka wakazi wa wilaya hiyo, kuanza kutumia vizuri mvua zinazonyesha kwa kuandaa mashamba ya mazao ya chakula na malisho ya mifugo.

“Huu ni wakati wa kuweka mikakati imara ya kuongeza uzalishaji, tuzitumie vizuri mvua zilizopo” alisema

Kaimu Ofisa Kilimo Wilaya ya Monduli, Theobald Ngobya alisema kutokana na uhaba wa mvua msimu uliopita wilaya hiyo inahitaji tani 28000 za chakula.

“Tunawataka wananchi kutumia vizuri mvua ambazo zimeanza kunyesha ili kuandaa mashamba na kukabiliana na upungufu wa chakula” alisema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live