Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yaua 11 Morogoro, majina yao yatajwa

Wed, 16 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kufuatia mvua za Vuli zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, mkoani Morogoro mvua hizo zimesababisha vifo vya watu 11 kati yao ni watoto tisa wenye umri kati ya miaka 11 hadi 15.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa ametoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 15, 2019.

Mutafungwa amesema tukio la kwanza ni la  watoto watano waliofariki baada ya kuzama katika mto Mvuha uliopo kata Kibogwa Tarafa ya Matombo wilaya ya Morogoro .

Amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 12, 2019 majira ya saa 16.30 jioni huko katika kijiji cha Nyachiro, kata ya Kibogwa Tarafa ya Matombo, wilaya ya Morogoro.

Aliwataja watoto hao ni Neema Rajabu (10) Latifa Khalid (9) wote wawili ni wanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Nyachiro huku  Munila Khalid (11) mwanafunzi wa darasa tatu katika shule hiyo hiyo pamoja na Omary Khalid (14) .

Kamanda huyo amesema miili ya watoto hao wanne ilipatikana huku  Zanisha Adam (9) mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Nyachiro  mwili  wake bado haujapatikana na shughuli ya uokoaji inaendelea kwa kushirikiana na polisi na kikosi cha uokoaji cha zimamoto wilayani humo.

Pia Soma

Advertisement
“Said Rajabu (11) mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi Nyachiro ambaye naye alikuwa na wenzake hao waliofariki, yeye alifanikiwa kukimbia baada ya kuona maji yanazidi kuwa mengi.”

“Alianguka na kuumia usoni na mkononi, anaendelea na matibabu katika zahanati ya Kibogwa,” amewema kamanda huyo.

Kamanda Mutafungwa amesema tukio la pili limetokea Oktoba 13, 2019 saa 12 asubuhi huko katika Bwala la Mindu Manispaa ya Morogoro, kamanda huyo amesema Jabiru Chris (40) mvuvi mkazi wa Manzese alifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye bwawa hilo akiwa katika shughuli za uvuvi.

Amesema  chanzo cha kifo chake ni mtumbwi aliokuwa akitumia katika shughuli zake za uvuvi ulipoteza mwelekeo kisha kuzama katika maji na kusababisha kifo hicho ambapo mwili wake umehifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa wa Morogoro.

Katika tukio la tatu kamanda huyo amewataja Rajabu Issa (11) na mwenzake Shabani Msimbe (15)  wanafunzi wa shule ya msingi Kibwaya, Tarafa ya Mkuyuni  walifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye dimbwi la maji walilokuwa wakiogelea.

Kamanda huyo amesema tukio hilo limetokea Oktoba 11, 2019 saa 8.00 mchana katika kitongoji cha Kisemo, kijiji cha Kibwaya  Tarafa ya Mkuyuni, ambapo maji hayo yalitokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani hapa.

Katika tukio la nne, limelokea Oktoba 6, 2019 saa 4 asubuhi Kipera, kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro ambapo kamanda huyo amesema Yasin Ally (50) mkazi wa Kipera, alifariki dunia baada ya kutumbukia kwenye dimbwi la maji alilokuwa akiogelea.

Kamanda huyo amesema Oktoba 5, 2019 saa 6 mchana  katika kitongoji cha Ulundo, kijiji cha Mtego wa Simba , kata ya Mikese wilaya ya Morogoro, Karimu Athuman (13) na Hussein Hassan (14) wanafunzi wa shule ya msingi Ulundo walifariki dunia kwa kuzidiwa na maji wakiwa mto Ngerengere  wakati wakiogelea.

Wakati huo huo, kamanda huyo amesema watu wawili  Ramadhani Mkuku na Frank Daud walifariki dunia katika kiwanda cha Sukari cha Kilombero K2  baada ya kutumbukia  katika bwawa la kuhifadhia uchafu utokanao na miwa.

Kamanda huyo amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 14, 2019 katika kiwanda cha Sukari cha K2 kata ya Ruaha, tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa, ambapo watu hao walikuwa wakijaribu kuiba Molasisi hivyo kuteleza na kutumbukia na kufariki dunia.

Chanzo: mwananchi.co.tz