Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yatikisa Morogoro, wananchi wavushwa kwa kamba

Mvua Morogoroooo.png Mvua yatikisa Morogoro, wananchi wavushwa kwa kamba

Tue, 30 Jan 2024 Chanzo: mwanachidigital

Askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, wamelazimika kuwavusha kwa kamba wananchi wanaotumia barabara ya Mazimbu iliyopo Kata ya Kihonda na Lukobe na wengine kuwabeba watoto baada ya barabara hiyo kujaa maji eneo la 'Kwa bwanajela'.

Tukio hilo limetokea leo asubuhi, Januari 30, 2024 baaad ya mvua kunyesha na kusababisha wananchi kushindwa kwenda kwenye shughuli zao za kila siku na wanafunzi kwenda shule.

Tangu Januari 5, 2024 yalipotokea mafuriko mkoani hapa, mvua kubwa zimekuwa zikiendelea kunyesha na kusababisha barabara hiyo kugeuka mto, huku barabara nyingine za kata hiyo zikikatika na kushindwa kupitika kabisa.

Mmoja wa wananchi waliokutwa wakivushwa, Shani Ally amesema kwa muda mrefu eneo hilo limekuwa korofi na kwamba kwa mvua za mwaka huu hali imekuwa mbaya zaidi.

"Mvua ya jana ilianza saa 11 jioni na haijakatija mpaka muda huu saa 3 asubuhi, nimelazimika kumpeleka mtoto wangu shule kwa kuwa hakuna gari inayopita hapa," amesema Shani.

Diwani wa Lukobe, Selestine Mbilinyi amesema mvua za mwaka huu zimeleta madhara makubwa kuliko zilizotokea miaka ya nyuma.

"Watu wamepoteza maisha, makazi, mali na hata miundombinu nayo imeharibika kwa kiasi kikubwa,” amesema na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu huku akiwasisitiza kuchukua tahadhari, ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Ameishukuru Serikali ya Wilaya na Mkoa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua za haraka zilizochukuliwa ambazo zimepunguza madhara.

Maeneo mengine yaliyoathirika na mvua hiyo katika Manispaa ya Morogoro ni pamoja na Mkundi, Lugala, Kasanga, Bigwa, Mafisa na Mwembesongo.

Chanzo: mwanachidigital