Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yasababisha walimu na wanafunzi kuhamishwa shule

A73bea5ed292e82ed7a380fbee63c7f1.jpeg Mvua yasababisha walimu na wanafunzi kuhamishwa shule

Mon, 10 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MANISPAA ya Bukoba imewahamisha wanafunzi 327 na walimu tisa wa Shule ya Msingi Nyamukazi kutokana na shule hiyo kuzungukwa na maji.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wazazi wa watoto wamekuwa wakiwabeba watoto wao mgongoni kwa wiki mbili sasa kuwapeleka shule.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Benard Limbe, wanafunzi wa shule hiyo wamehamishiwa katika Shule ya Msingi Tumaini iliyokuwa na vyumba saba visivyotumika.

Kuhamishwa kwa wanafunzi hao kunaongeza mwendo wa kilometa mbili kutoka Shule ya Msingi Nyamukazi hadi Tumaini ambayo ilijengwa upya kupisha safari za ndege katika kiwanja cha ndege kilichopo katika Manspaa ya Bukoba.

Hata hivyo, Shule ya Msingi Nyamukazi hutumiwa na wanafunzi pia ambao hutoka katika Kisiwa cha Musira kilichopo Manispaa ya Bukoba ambao nao hulazimika kutumia boti kwa ajili ya kwenda shuleni.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, si mara ya kwanza shule hiyo kujaa maji kutokana na kuwa kandokando mwa Ziwa Victoria na kuathirika mvua kubwa zinaponyesha.

“Tulikuwa tukimwaga vifusi vingi ili kuongeza uwezekano wa wanafunzi kupita na kuendelea kupata elimu, lakini hizi mvua zimenyesha mfululizo wiki mbili na maji yamemeza vifusi vyote, tunaona ni bora wanafunzi wahame kwanza ili kutafuta ufumbuzi,” alisema Limbe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz