Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yasababisha mafuriko wilayani Korogwe

81772 Mafuriko+pic Mvua yasababisha mafuriko wilayani Korogwe

Sat, 26 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Mvua inayoendelea kunyesha mkoani Tanga imesababisha baadhi ya nyumba katika Wilaya ya Korogwe kuzingirwa na maji.

Kuanzia leo Jumamosi Oktoba 26, 2019 nyumba hizo zilianza kujaa maji kutokana na Mto Pangani kujaa maji na kuelekea kwenye makazi ya watu.

Mwananchi limeshuhudia baadhi ya wananchi wakiokoa samani mbalimbali katika nyumba zao.

Zainabu Said amesema maji yalianza kuingia katika nyumba yake asubuhi na kuharibu vitu vingi, “inanibidi nihame leo kuokoa vitu vyangu, siwezi kukaa tena hapa.”

Naye Juma Hamis amesema mvua imewapa hasara, “tunaomba msaada wa Serikali kwani tumepata hasara kubwa.”

Hadi leo saa 4:30 asubuhi  mamia ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani na waliotoka Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali  wamekwama wilayani hapo  tangu jana mchana Ijumaa Oktoba 25, 2019.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Wamekwama kutokana na maji kupita juu ya daraja la Mandera na kulisomba daraja la Handeni mkoani humo.

Wakizungumza na Mwananchi,  Jane Mathias na Juma Kombo wamesema tangu jana saa 5 asubuhi wamekwama katika daraja hilo kutokana na wingi wa maji uliotokana na mvua inayoendelea kunyesha mkoani Tanga.

"Tumefika hapa jana saa 5 asubuhi hadi muda huu (leo saa1 asubuhi) hatuoni uwezekano wa kuvuka," amesema Mathias.

Kombo ameiomba Serikali kuondoa adha hiyo kwa sababu kwa wiki mbili sasa daraja la Mandera limekuwa likijaa maji.

"Ni aibu barabara muhimu kama hii watu kukwama kutokana na daraja kujaa maji, kila siku wanajenga vivuko hawaimarishi  barabara," amesema Mathias.

Musa Mposi, mkazi wa kijiji cha kwa Kombo jirani na daraja hilo amesema ni mara ya kwanza kujaa maji.

"Hii barabara ilikuwa nzuri ila ukarabati uliofanywa hivi karibuni ndio umeongeza tatizo" amesema Mposi.

Akizungumza na Mwananchi asubuhi hii, kuhusu athari zilizotokea hadi sasa ikiwamo vifo, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Kissa Mwangoka amesema maafa lazima yatakuwapo kwa sababu mvua inayoendelea kunyesha ni kubwa sana.

“Hali ya sasa maji yanapungua eneo la Mandera liliko Daraja la Mandera lakini bado hakupitiki,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz