Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yaleta maafa, 200 waathiriwa Shinyanga

Mvua Yawatenga Wananchi Wa Kata Ya Maboga Na Wengine Mvua yaleta maafa, 200 waathiriwa Shinyanga

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya wakazi 200 wa vijiji vya Bugayambelele na Bujinge Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga wameathiriwa na mvua iliyoambana na upepo ulioezua na kuangusha nyumba zaidi ya 70 walizokuwa wakiishi.

Mvua hiyo ilianza kunyesha saa 5.00 usiku wa kuamkia leo Jumapili, Machi 3, 2024 ikiambatana na upepo mkali.

Waathirika wa mvua hiyo akiwemo John Songolo, wameiomba Serikali kuwasaidia kupata hifadhi ya muda.

Songolo amesema nyumba yake imeanguka akiwa ndani, alianza kusikia upepo mkali na ghafla matofali yakaanza kuanguka, kisha ukuta ukaanguka lakini aliweza kuokolewa.

Ameiomba Serikali kuwasaidia chakula na hifadhi, kwani kwa sasa hawana mahali pa kuishi.

Neema Rukibanzi, mkazi wa Kijiji cha Bugayambelele amesema alikuwa na kuku 1,000 kwenye banda, amefanikiwa kuokoa kuku 700, huku 300 wakifa baada ya banda lake kuezeliwa na upepo mkali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugayambelele, Emmanuel William amesema maafa ni makubwa kutokana na athari za mvua iliyonyesha.

Amesema kaya nyingine nyumba zimebomoka zote, hivyo kukosa makazi.

Diwani wa Kizumbi, Reuben Kitinya, amesema mvua imeathiri vijiji viwili vya Bugayambelele na Bujinge. Pia imeathiri baadhi ya nyumba za ibada ambazo zimeezuliwa.

Kitinya amesema katika Kijiji cha Bugayambelele kaya nane hazina makazi na kwenye Kijiji cha Bujinge kaya 11 hazina pakuishi.

Amesema nyumba zilizoanguka na kuezuliwa mapaa ni 72 kwenye vijiji vyote viwili.

Mratibu wa maafa Mkoa wa Shinyanga, Revocatus Lutunda amesema kamati za maafa ngazi ya wilaya na kata zinaendelea kuchukua takwimu za waathirika, ili kutoa huduma za kibinadamu.

Amewaomba wananchi wenye nafasi kuwasaidia wahitaji kwa kuwapatia hifadhi.

Amesema kaya zote zilizoathirika na mvua zinakadiriwa kuwa na watu zaidi ya 200.

Lutunda amebainisha kuwa mpaka sasa hakuna kifo kilichotokea kutokana na maafa ya mvua hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live