Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yakwamisha magari nane ya misiba Kilimanjaro

Mvua Yawatenga Wananchi Wa Kata Ya Maboga Na Wengine Mvua yakwamisha magari nane ya misiba Kilimanjaro

Sat, 25 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Same. Mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Kilimanjaro, zimesababisha kukatika kwa mawasiliano eneo la Hedaru, wilayani Same, hali ambayo imesababishwa magari yaliyokuwa yamebaba miili ya marehemu kuja mkoani Kilimanjaro, kushindwa kuendelea na safari.

Changamoto hiyo ilitokea jana usiku, Novemba 23, baada ya mafuriko kusomba mawe na magogo kutoka maeneo ya milimani na kusababisha kuziba kwa barabara kuu ya Moshi - Dar es Salaam na kusababisha magari kushindwa kupita usiku kucha.

Akizungumza leo Ijumaa, Novemba 24 katika mkutano wa waandishi wa habari, Mkuu wa mkoa huo, Nurdin Babu amesema wamefanikiwa kuondoa mawe na magogo yaliyokuwa yameziba katikati ya barabara na kwamba asubuhi magari yalianza kupita.

"Jana mvua kubwa imenyesha maeneo ya milimani kule Same, imeporomosha mawe na magogo na kuanzia jana saa saba usiku, hakuna gari ambalo liliweza kupita kuja Moshi, wananchi walikwama eneo hilo, magari kama nane yaliyokuwa yamebeba misiba kuja kuzika yalishindwa kupita, maiti zilikuwa pale, kwa hiyo tumekwenda tumeshughulikia tatizo sasa hivi magari yanapita vizuri,"

"Tulimtuma Meneja wetu wa Tanroad mkoa amekwenda na mimi na kamati yangu ya usalama tumekwenda kule asubuhi na kazi kubwa na nzuri imefanyika na magari yanapita bila changamoto yoyote," amesema RC Babu.

Babu amewaomba wananchi wanaoingia mkoani humo kuendelea kuwa watulivu wakati wa changamoto hii ya mvua na kwamba wamepeleka vifaa na wameweza kuondoa magogo na mawe hayo na barabara zinapitika.

Naye, Mkuu wa wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema kwasasa hali ni shwari na magari yanapita bila changamoto yoyote katika eneo hilo baada ya kufanikiwa kuondoa magogo na mawe hayo ambayo yalitokea maeneo ya milimani kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live