Mamia ya wasafiri waliokuwa wakisafiri kutoka nje ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kwenda maeneo mbalimbali nchini wamekwama kwa zaidi ya saa nane katika eneo la Kwa Msomali, wilayani humo baada ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara yaliyosababishwa na Mto Sanya kujaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kutokana na hali hiyo, imesababisha magari yote yanaoingia na kutoka Kilimanjaro katika barabara kuu ya Moshi-Arusha kushindwa kuendelea na safari kutokana na kukatika kwa mawasiliano hayo ya barabara.
Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema changamoto hiyo imejitokeza tangu usiku wa saa 7 ya Jumapili Aprili 14, 2024 kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
"Ni kweli kumetokea changamoto hapa Sanya tangu saa 7 usiku na tuko hapa muda huu, tunashughulika na hii changamoto kuona ni namna gani magari yanaweza kupita," amesema.
Hata hivyo, amesema chanzo ni magogo kuziba daraja hilo ambapo amesema baada ya magogo kuondolewa katika eneo hilo magari yameshaanza kuruhusiwa kupita upande mmoja kuendelea na safari.